Skip to main content
News and Events

ZAIDI YA WAJASIRIAMALI 300 WASHIRIKI MAONESHO YA JUAKALI UGANDA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanikisha ushiriki wa Wajasiriamali zaidi ya 300 katika maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu Juakali yanayofanyika katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda kuanzia terehe 8 - 18 Disemba 2022.

Maonesho hayo yanayoongozwa na kauli mbiu “Nunua Bidhaa za Afrika Mashariki, ili kujenga Uchumi Stahimilivu na Endelevu wa Afrika Mashariki” yanalenga kutoa fursa kwa Wajasiriamali ya kuonesha huduma na bidhaa mbalimbali wanazozalisha na kubadilishana uzoefu, ujuzi na taarifa na wajasiriamali wenzao katika Jumuiya, sambamba na kukuza wigo wa masoko mapya.

Maonesho hayo ambayo yamevutia Wajasiriamali zaidi 1500 kutoka Nchi zote saba (7) Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, na ikikadiriwa 75% kati yao kuwa ni wanawake, yamesheheni bidhaa mbalimbali zenye asili ya Jumuiya. Kwa upande wa wajisiriamali wa Tanzania miongoni mwa bidhaa na huduma wanazozionesha ni pamoja na mavazi ya asili, bidhaa za baharini, bidhaa za kilimo zilizoongezewa thamani, mashine za kuzalisha bidhaa mbalimbali, madawa ya asili, vito vya thamani na madini, utalii, na bidhaa za ngozi kama vile viatu, mabegi na mikoba.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Wajasiliamali wa Tanzania wameonesha kuridhishwa kwao na kupongeza juhudi na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania chini ya Uongozi madhubuti wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya biashara ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kushiriki katika maonesho hayo.

“Kutokana na gharama kubwa za kusafirisha bidhaa zetu hadi hapa nchini Uganda, wengi wetu tusingeweza kumudu, hivyo tusingeweza kuwa na uwakilishi wa kutosha katika maonesho haya. Hata hivyo kutokana na dhamira ya Serikali ya kutusaidia wajasiriamali kukua kibiashara kupitia kupata masoko mapya ya huduma na bidhaa tunazozalisha na kutuongezea ujuzi na uzoefu imeona ni vyema ituwezeshe katika maeneo mbalimbali ikiwemo kugharamia usafiri wa kutuleta hapa nchini Uganda na kuturudisha nyumbani baada ya maonesho”. Ameeleza Lilian Sambu mjasiliamali.

Maonesho ya Juakali yalifanyika kwa mara ya kwanza mwezi Novemba 1999 jijini Arusha, ambapo yaliambatana na tukio la kihistoria la kusainiwa kwa Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika maonesho hayo, Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki walielekeza kuwa yafanyike kila mwaka kwa mzunguko kati ya Nchi Wanachama ili kuimarisha mtangamano wa jamii na uchumi wa watu wa Afrika Mashariki.

 

  • Bw. Joseph Ndunguru (kulia) mzalishaji wa bidhaa za vyakula kutoka mjini Mtwara akielezea bidhaa zake kwa mteja aleyetembelea banda lake kwenye maonesho ya 22 ya Juakali yanayoendelea katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda.
  • Wateja wakichangamkia bidhaa za mmoja wa wajasiriamali wa Tanzania (kulia) walipotembelea banda lake katika maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu Juakali yanayoendelea katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda.
  • Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza na Waziri anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki wa Uganda Mhe. Rebecca Alitwala Kadaga (mwenye chupa ya mvinyo mkononi) akipokea zawadi kutoka kwa mmoja wa wajasiriamali wa Tanzania kwenye maonesho ya 22 ya Juakali yanayoendelea jijini Kampala, Uganda
  • Mkurugenzi Msaidizi wa Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji Bw. Athuman Nkungu akiangalia bidhaa ya mmoja wa wajasiriamali alipotembelea meza yake kweye maonesho 22 ya Juakali yanayoendelea katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda
  • Sehemu ya wajasiriamali wa Tanzania wakimsalimia Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza na Waziri anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki wa Uganda Mhe. Rebecca Alitwala Kadaga (yupo kwenye gari inayoonekana pichani) alipotembelea banda la Tanzania kweye maonesho 22 ya Juakali yanayoendelea katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda
  • Mkurungenzi wa Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,Ajira,Vijana na Wenye Uemavu) Bw. Ally Msaki akizungumza na Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza na Waziri anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki wa Uganda Mhe. Rebecca Alitwala Kadaga alipotembelea banda la Tanzania kwenye maonesho ya 22 ya Juakali yanayoendelea jijini Kampala, Uganda
  • Naibu Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala Mhandisi Steven Mlote akifuatilia maelezo ya mjasirimali alipotembelea banda la Tanzani kwenye maonesho ya 22 ya Juakali yanayoendelea katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda
  • Mkurugenzi Mtendaji wa Just Products Bi. Judith M. Lugembe akifuatilia taarifa ya biashara yake katika maonesho ya 22 ya Juakali yanayoendelea katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda
  • Sehemu ya wajasiriamali wa Tanzania wakipanga bidhaa zao kweye maonesho 22 ya Juakali yanayoendelea katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda