Skip to main content
News and Events

WIZARA YA MAMBO YA NJE NI KATI YA WIZARA 14 NA TAASISI 60 ZINAZOSHIRIKI MAONESHO YA UTUMISHI WA UMMA

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeshauriwa kuangalia uwezekano wa kujenga Kituo cha Kimataifa cha Mikutano jijini Dodoma kufuatia jiji hilo kukua kwa kasi na Serikali kujenga miundombinu ya kisasa, yenye ubora wa hali ya juu.
Ushauri huo umetolewa leo Juni 19, 2024 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Goerge Simbachawene (Mb) alipotembelea Banda la Wizara katika Maonesho ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika kwenye Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Akitoa taarifa kuhusu ushiriki wa Wizara katika Maonesho hayo, Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Noel Kaganda alimwambia Mhe. Waziri Simbachawene kuwa Wizara kwa sasa, kwa kushirikiana na Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) inaendelea na mchakato wa kujenga Kituo kipya cha Mikutano jijini Arusha ambacho kinatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano mkubwa wa APIMONDIA Unaohusu ufugaji wa nyuki unaotarajiwa kufanyika Arusha mwaka 2027 na utahusisha wadau zaidi ya 6000.

Waziri Simbachawene ambaye alikuwa Mgeni rasmi katika ufunguzi wa maonesho hayo alitoa wito kwa watumishi na wananchi kwa ujumla kuwa na mwamko wa kutumia mifumo ya TEHAMA inayoanzishwa na taasisi za umma kwa lengo la kurahisisha utoaji wa huduma na kuondoa ukiritimba na urasimu.

“Taasisi za umma takribani zote nchini zina mifumo ya TEHAMA ya kutoa huduma lakini mwamko kwa wananchi bado sio mzuri wa kutumia mifumo hiyo ambayo lengo lake ni kuharakisha huduma na kuwaondolea usumbufu wananchi” Waziri Simbachawene alisema.

Waziri Simbachawene alihitimisha hotuba yake kwa kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika maonesho hayo ambayo yatafungwa tarehe 23 Juni 2024 ili waweze kupata huduma za papo kwa papo na taasisi zinazoshiriki ikiwa ni pamoja na kupata hati za viwanja, vitambulisho vya taifa na kupima afya.

Wizara na taasisi zake za AICC, Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim na Mpango wa Afrika Kujitathimini Kiutawala Bora (APRM-Tanzania) ni kati ya Wizara 14 na taasisi 60 zinazoshiriki maonesho hayo.