Dkt. Salem Al-Junaibi (Mb) na Ujumbe wake Awasili nchini kwa Ziara ya Kibiashara
Dkt. Salem Al-Junaibi (Mb), Mjumbe wa bodi ya wakurugenzi wa Chama cha Biashara na Viwanda cha Oman akiongoza ujumbe wa Wafanyabiashara kutoka chama cha wafanyabiashara na wenye viwanda cha Oman, amewasili nchini leo, tarehe 7 Septemba 2025, kwa ziara ya siku tano, kuangazia fursa za uwekezaji na biashara za Tanzania, katika sekta mbalimbali.
Ziara hii ni moja ya juhudi za Serikali za Tanzania na Oman kukuza biashara.
Itakumbukwa Mwezi Mei 2025, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Hashil Twaibu, alifanya ziara rasmi nchini Oman akiambatana na viongozi wa chama cha wafanyabiashara na wenye viwanda, kilimo cha Tanzania kwa madhumuni makubwa ya kuimarisha uhusiano katika sekta ya biashara na uwekezaji kati ya nchi hizi mbili.
Mara baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dkt. Al-Junaibi na ujumbe wake, alipokelewa na Mhe. Dkt. Hashil Twaibu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, pamoja na Balozi Abdalah Kilima, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Viongozi wengine waliompokea ni Rashid Al Mandhir, Naibu Balozi wa Oman nchini Tanzania, Ndugu Oscar Kisanga, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wafanyabiashara, viwanda na kilimo Tanzania pamoja na Maafisa Waandamizi wa Serikali na Sekta binafsi.
Katika ziara yao, Dkt. Al-Junaibi na ujumbe wake wanatarajiwa kukutana na viongozi wa Serikali pamoja na taasisi mbalimbali za umma na binafsi, zikiwemo chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), TISEZA, BRELA, TANTRADE, TBS, TIRDO na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC).
Aidha, ujumbe huo pia utatembelea Kiwanda cha Nyama cha Union Meat – Kibaha, Eneo la viwanda (Industrial Park) KAMAKA, Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), pamoja na Bodi ya Chai Tanzania (TBT).
Vilevile ujumbe huo pia utashiriki katika mazungumzo na Makatibu Wakuu wa Wizara za Viwanda na Biashara, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Nishati, pamoja na Ofisi ya Rais – Kazi, Uchumi na Uwekezaji.
Katika mikutano hiyo, Chama cha Wafanya biashara, Viwanda na Kilimo cha Tanzania (TCCIA) na Chama cha Wafanyabiashara na Viwanda cha Oman (OCCI) zitasaini mikataba wa ushirikiano baina yao.
Dkt. Al-Junaibi na ujumbe wake pia watatembelea Zanzibar ambako watakutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa ZIPA, ZNCC, pamoja na kutembelea Eneo Maalum la Uchumi Zanzibar.
Mbali na mazungumzo hayo na Serikali ya Tanzania Bara na Zanzibar, ujumbe huo wa wafanyabiashara wa Oman pia utafanya mawasilisho kuhusu hali ya biashara na viwanda nchini Oman, pamoja na fursa mbalimbali za ushirikiano wa kibiashara kati ya Oman na Tanzania.
Ziara hiyo ya Dkt. Al-Junaibi na ujumbe wake inatarajiwa kukamilika tarehe 12 Septemba, 2025, kabla ya kurejea nchini Oman.