Skip to main content
News and Events

WAZIRI MULAMULA AFANYA ZIARA KATIKA MAHAKAMA YA KIMATAIFA YA KESI MASALIA ZA MAUAJI YA KIMBARI (IRMC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula amefanya ziara ya kikazi katika Mahakama ya Kimataifa ya Kesi Masalia za Mauaji ya Kimbari (IRMCT) tarehe 21 Mei 2022 katika eneo la Lakilaki, jijini Arusha.

Pamoja na mambo mengine dhumuni la ziara hiyo lilikuwa kukutana na Uongozi wa IRMCT na kujadili utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya kimsingi unaofanywa na taasisi hiyo sambamba na yale ya kimahakama.

Waziri Mulamula alitumia nafasi hiyo kueleza kuwa Tanzania inathamini imani inayotolewa na mashirika ya kimataifa pamoja na kikanda ya kuifanya kuwa mwenyeji wa mashirika hayo na kutoa nafasi za ajira kwa Watanzania.

‘’ Serikali inafuatilia kwa karibu utendaji kazi wa Mahakama hii, hivyo ni vema mkatekeleza kwa tija malengo mahsusi ya kuanzishwa kwake,” alisema Balozi Mulamula.

Pia akasisitiza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo tayari kutoa ushirikiano wa kiutendaji wakati wowote itakapohitajika ili kuiwezesha Mahakama kutekeleza majukumu yake ya msingi ikiwemo kukamilisha taratibu za kesi zilizosalia na lile la kuwa kituo cha kumbukumbu kwa kesi hizo linatekelezwa kwa ufanisi.

Naye Msajili wa Mahakama hiyo Bw. Abubaccar Tambadou amemshukuru Mheshimiwa Waziri Mulamula kwa kuthamini Mahakama hiyo na kutenga muda wake kujadili masuala mbalimbali ya kiutendaji.

Pia akaeleza kuwa kikao hicho kimewezesha kupatikana kwa ufumbuzi wa papo kwa papo katika baadhi ya mambo na kuleta uelewa wa pamoja kati ya uongozi wa Mahakama na Serikali mwenyeji juu ya masuala ya kiutendaji wa taasisi hiyo.

Naye Jaji wa Mahakama hiyo Mheshimiwa William Sekule alifafanua kwa kina juu ya utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya kimahakama na pia akaeleza kuwa kufanikiwa kwa Mahakama hiyo kunahitaji msaada kutoka kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa na nchi mwenyeji katika kutetea maslahi mbalimbali kwa ajili ya kuwezesha uendeshaji wa shughuli za taasisi.

‘’Naipongeza Tanzania kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kupigania upatikanaji wa bajeti ya uendeshaji wa Mahakama, hivyo ni vema tukatambua thamani ya mahakama hii kuendelea kuwepo nchini na kukamilisha majukumu yake,” alisema Jaji Sekule.

Tangu Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa lipitishe Azimio Nambari 1966 mwaka 2010 la kuanzisha Mahakama hiyo nchini, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilisimamia hatua mbalimbali za awali ili kuhakikisha ujenzi wa Mahakama hii unakamilika hususan upatikanaji wa eneo la ujenzi, uwepo wa huduma ya umeme, barabara na maji katika eneo la Lakilaki Jijini Arusha.

  • Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) akifafanua jambo wakati wa kikao na Uongozi wa Mahakama ya Kimataifa ya Kesi Masalia za Mauaji ya Kimbari kilichofanyika tarehe 21 Mei 2022 katika eneo la Lakilaki, jijini Arusha. Pembeni ya Mhe. Waziri ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Caroline Chipeta.
  • Waziri Mulamula akipata maelezo katika chumba cha Mahakama na taratibu nyingine za uendeshaji wa kesi katika mahakama hiyo.
  • Kikao kikiendelea