Skip to main content
News and Events

WAZIRI MKUU WA ETHIOPIA ATUA NCHINI KWA ZIARA YA KITAIFA YA SIKU TATU

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia, Mhe. Dkt. Abiy Ahmed Ali amewasili nchini leo tarehe 29 Februari 2024 kuanza ziara yake ya  kitaifa ya siku tatu.

Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Mhe. Waziri Mkuu Abiy amepokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba.

Mhe. Dkt. Abiy atapokelewa rasmi na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam tarehe 01 Machi 2024.

Pamoja na mambo mengine ziara ya Waziri Mkuu Abiy inalenga kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Ethiopia katika maeneo ya kimkakati ikiwemo usafirishaji kwa njia ya anga, nishati, kilimo na mifugo, biashara na uwekezaji na Ushirikiano katika sekta za elimu, uhamiaji, na ulinzi na usalama 

Ziara hiyo ambayo itakamilika tarehe 02 Machi 2024 inafanyika kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

  • Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba (Mb.) akisalimiana na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Dkt. Abiy Ahmed Ali mara baada ya kuwasili Tanzania kwa ziara ya Kitaifa ya siku tatu.
  • Mhe. Dkt. Abiy Ahmed Ali akishuka kwenye ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.
  • Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Dkt. Abiy Ahmed Ali akisalimiana na Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Mhe. Innocent Shiyo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.