Waziri aongoza ujumbe wa Mawaziri wa Asasi ya SADC nchini DRC
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Mhe Augustine Mahiga yupo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 10 hadi 13 Oktoba, 2016.
Mhe. Mahiga ambaye anaongoza ujumbe wa Mawaziri wa Asasi hiyo yupo nchini humo kwa maagizo ya Mwenyekiti wa Asasi, Mhe. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kutathmini hali ya siasa ilivyo nchini humo ili kushauri ipasavyo.
Aidha, tathmini hiyo inafanyika kufuatia hali tete ya kisiasa, kiulinzi na kiusalama nchini DRC iliyochangiwa na maandamano yaliyofanyika tarehe 19 Septemba, 2016 ambayo yaliandaliwa na vyama vya upinzani kwa lengo la kushinikiza Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya DRC (CENI) kutangaza tarehe ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu.