Skip to main content
News and Events

UINGEREZA IMEIPONGEZA TANZANIA KWA KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA, UWEKEZAJI, HAKI ZA BINADAMU

UINGEREZA IMEIPONGEZA TANZANIA KWA KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA, UWEKEZAJI, HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Uingereza imeipongeza Tanzania kwa jitihada zake za kuboresha mazingira ya biashara, uwekezaji, Haki za Binadamu na Utawala Bora, jambo ambalo limeimarisha ushirikiano baina ya Nchi hizo. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) ameyasema hayo wakati wa mazungumzo kwa njia ya mtandao na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza anayeshughulikia Masuala ya Afrika, Jumuiya ya Madola na Maendeleo Mhe. James Duddridge, ukiwa ni utekelezaji wa mazungumzo ya awali kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri huyo alipofanya ziara hapa nchini

Balozi Mulamula ameongeza kuwa kutokana na mazungumzo hayo Uingereza na Tanzania zimekubaliana kufanya kongamano kubwa litakalojumuisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Uingereza ili kuja kuwekeza hapa nchini. 

Pia Balozi Mulamula ameishukuru Uingereza kwa kuiunga mkono Tanzania katika bodi ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) jambo lililoiwezesha Tanzania kupata mkopo wa masharti nafuu wa shilingi Trilioni 1.3 kwa ajili ya kukabiliana na adhari za UVIKO 19.

Katika tukio jingine Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amekutana kwa mazungumzo na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bi. Clementine Nkwera-Salami, ambapo ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kulisaidia Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) ili kuliwezesha kutekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwemo kuwarejesha wakimbizi makwao kwa hiari.

 “Ili shirika hili liendelee kuhudumia vyema wakimbizi ni muhimu Jumuiya ya Kimataifa ikaendelea kutoa mchango wake, hasa kwa kuwaongezea bajeti UNHCR ambayo itawawezesha kutimiza majukumu yao kwa wakati na kwa ufanisi zaidi” alisema Mheshimiwa Balozi Mulamula 

Kwa upande wake Mkurugenzi huyo wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bi. Clementine Nkwera-Salami kwa niaba ya Shirika hilo ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watanzania kwa kuendelea kutoa mchango wa muda mrefu katika kutafuta suluhisho la kudumu kwa wakimbizi. 

Ofisi ya Kikanda ya UNHCR iliyopo Kasulu, Kigoma inahudumia nchi Kumi na Moja (11) ambazo ni; Burundi, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somalia, South Sudan, Tanzania and Uganda.

  • Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bi. Clementine Nkwera-Salami wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa Wizara na Watendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi.
  • Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bi. Clementine Nkwera-Salami akielezea jambo wakati wa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula yaliyofanyika jijini Dodoma.
  • Mazungumzo yakiendelea
  • Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akijadili jambo na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika Bw. Gerald Mbwafu baada ya kumaliza mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza anayeshughulikia Masuala ya Afrika, Jumuiya ya Madola na Maendeleo Mhe. James Duddridge.
  • Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo kwa njia ya mtandao na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza anayeshughulikia Masuala ya Afrika, Jumuiya ya Madola na Maendeleo Mhe. James Duddridge.
  • Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bi. Clementine Nkwera-Salami (kushoto) wakiwa katika mazungumzo yaliyofanyika jijini Dodoma