Skip to main content
News and Events

TANZANIA, NORWAY KUSHIRIKIANA KUIMARISHA UCHUMI

Serikali za Tanzania na Norway zimesisitiza kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo ili kukuza uchumi.

Msisitizo huo umetolewa wakati wa mazungumzo ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb.) na Waziri wa Norway anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa na nchi za Nordic, Mhe. Anne Beathe Tvinnereim walipokutana tarehe 06 Septemba 2022 katika ofisi ndogo za wizara Jijini Dar es Salaam.

Nchi hizo zinashirikiana katika masuala ya elimu, afya, kilimo, uwekezaji, miundombinu, nishati, madini, tehama, utafiti, maboresho kwenye mifumo ya ukusanyaji wa kodi, uchangiaji wa bajeti kuu ya Serikali, misitu, demokrasia, haki za binadamu, usawa wa jinsia, utunzaji wa mazingira na ukuzaji wa sekta ya biashara.

Balozi Mulamula alieleza kuwa Tanzania inathamini ushirikiano uliopo baina yake na Norway kwa kusimamia miradi ya maendeleo iliyo kwenye makubaliano na kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano kwa lengo la kujenga uchumi wa Wananchi.

“Norway ni mshirika wa maendeleo wa Tanzania wa muda mrefu na imesaidia kujenga uwezo katika maeneo mbalimbali ya kiutendaji ikiwemo uboreshaji wa mazingira wezeshi ya uwekezaji na biashara, usimamizi wa mfumo wa ulipaji kodi,” alisema Balozi Mulamuala.

Kadhalika, Serikali ya Norway imeongeza muda wa miaka mitano ya utekelezaji wa makubaliano ya majadiliano ya kisiasa yaliyoingiwa kati yake na Tanzania yanaendelea ili kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya kipaumbele ya Serikali ya awamu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Doroth Gwajima alieleza kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na Norway katika utekelezaji wa pendekezo la mpango wa miaka mitano wa kujenga usawa na uwezo kwa wanawake, vijana na makundi maalum unaotegemewa kuinua uchumi na kuwawezesha kuajiriwa na kujiajiri katika kazi rasmi. 

Mpango huo pia umezingatia umuhimu wa  afya ya uzazi kuwa agenda muhimu ili kuyafikia Malengo ya Mpango wa Maendeleo Endelevu.

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Antony Mavunde alieleza kuwa kupitia sekta ya kilimo Tanzania inayo nia ya kushirikiana na Norway katika masuala ya kujenga uwezo katika vyuo vya kilimo na taasisi zake ili kuwezesha tafiti za sekta hiyo kwa lengo la kuinua uwezo binafsi wa kuzalisha mbegu za mazao, kusimamia usalama wa chakula nchini, kujenga mabwawa na kuimarisha miradi ya umwagiliaji.

Maeneo mengine ya ushirikiano ni pamoja na upatikanaji wa mbolea kwa gharama nafuu, uimarishaji na ujenzi wa miundominu ya kilimo ili kujenga uwezo wa kuzalisha kwa mwaka mzima badala ya kusubiri msimu wa mvua kama ilivyosasa.

Vilevile Wizara ya Kilimo imeandaa mpango wa miradi ya kilimo kwa Wanawake na Vijana itakayotekelezwa katika mikoa ya Mbeya na Dodoma ambapo mradi huo utatumia jumla ya ekari 69 hivyo, kupitia ushirikiano uliopo Tanzania ina dhamira ya dhati ya kushirikiana na Norway ili kuyafikia malengo ya uzalishaji yaliyowekwa katika kufanya kilimo cha biashara na kulifikia soko la kimataifa.

Naye Mhe. Tvinnereim ameeleza kuwa Norway imejenga uwezo mkubwa katika masuala ya uzalishaji wa mbegu hivyo itaendelea kushirikiana na Tazania katika eneo hilo na maeneo mengine yaliyoelezwa na mawaziri walioshiriki mazungumzo hayo kwa lengo la kuondoa umasikini, kuongeza nafasi za ajira na kujenga uwezo wa kiuchumi kwa wananchi.

  • Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Doroth Gwajima (Kushoto) akizungumza na ujumbe wa Norway ulioongozwa na Waziri wa Norway anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa na nchi za Nordic, Mhe. Anne Beathe Tvinnereim katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
  • Waziri wa Norway anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa na nchi za Nordic, Mhe. Anne Beathe Tvinnereim akipokea zawadi ya picha ya Mlima Kilimanjaro kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
  • Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Kushoto) akizungumza na ujumbe wa Norway ulioongozwa na Waziri wa Norway anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa na nchi za Nordic, Mhe. Anne Beathe Tvinnereim katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
  • Waziri wa Norway anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa na nchi za Nordic, Mhe. Anne Beathe Tvinnereim (Kulia) akizungumza na ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
  • Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Antony Mavunde akieleza jambo wakati wa mkutano baina ya Balozi Mulamula na Waziri wa Norway anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa na nchi za Nordic, Mhe. Anne Beathe Tvinnereim katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam