TANZANIA NA MAREKANI ZAKUBALIANA KUIMARISHA USHIRIKIANO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amepongeza kuimarika kwa ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Marekani hususan kwenye sekta zinazochangia kuboresha maisha ya watanzania kama afya, elimu, kilimo, miundombinu, usalama wa chakula, demokrasia na utawala bora.
Mhe. Dkt. Rais Samia ameyasema hayo wakati wa mkutano wa pamoja na Waandishi wa Habari uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam mara baada ya kumalizika kwa mazunguzo rasmi kati yake na Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.
Amesema kupitia ushirikiano na Marekani, magonjwa kama Kifua Kikuu na UKIMWI sio tishio tena hapa nchini kwani kupitia program mbalimbali zinazotekelezwa kwa ushirikiano baina ya nchi hizi mbili, kama Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR) maambukizi ya magonjwa haya kwa wananchi yamepungua kutoka asilimia 7.2 mwaka 2012 hadi asilimia 4.7 mwaka 2017.
Kuhusu vifo vitokanavyo na Malaria, Mhe. Dkt. Rais Samia amesema vimepungua kutoka milioni 7.7 mwaka 2015 hadi kufikia vifo milioni 3.5 mwaka 2021.
“Lengo letu ni kutokomeza malaria kabisa katika jamii yetu ya Tanzania. Pia tunakaribisha wawekezaji wenye tija kutoka Marekani kuwekeza kwenye viwanda vya utengenezaji wa dawa za kufubaza makali ya virusi vya UKIMWI ili zitengenezwe hapa nchini kwetu", amesema Mhe. Rais Dkt. Samia.
Mhe. Rais Dkt. Samia pia amesema anaikaribisha Marekani katika maeneo mapya ya ushirikiano hususan kwenye uvuvi katika bahari kuu, utafiti wa gesi na uchumi wa buluu.
Pia Mhe. Rais Samia ameiomba Marekani kupitia upya suala la utoaji visa ili kuwawezesha watanzania kupata visa za muda mrefu kwa ajili ya kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na huduma.
Kwa upande wake, Mhe. Kamala amesema Serikali ya Marekani inao Mpango mpya wa kushirikiana na Tanzania katika kusaidia miradi ya Teknolojia ya kidijiti, Usafirishaji na Nishati.
Amesema Serikali hiyo kupitia Benki ya Exim watasaini Hati ya Makubaliano na Tanzania ambayo itawezesha upatikanaji wa Dola za Marekani milioni 500 kugharamia upelekeaji wa huduma na bidhaa katika sekta za miundombinu, usalama wa mitandao, usafirishaji, teknolojia ya kidigiti, nishati na miradi ya nishati jadidifu.
Vilevile amempongeza Rais Samia kwa kuwa mstari wa mbele katika kuimarisha demokrasia nchini hususan kwenye masuala ya maridhiano na vyama vya siasa pamoja na kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari.
Amesema Marekani chini ya uongozi wa Mhe. Rais Joe Biden inaunga mkono agenda za kuimarisha Demokrasi anchini na itaendelea kushirikiana na Tanzania kwenye maeneo mbalimbali ya ushirikiano kama vile usalama wa chakula, afya, kuwasaidia wanawake na vijana Demokrasia na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Vilevile amesema katika kuimarisha ushirikiano na Tanzania, Marekani ina mpango wa kujenga kiwanda kikubwa cha kuchakata madini ya nikeli yanayotumika kutengeneza betri za umeme wa magari ifikapo mwaka 2026.
Mhe. Kamala ameishukuru na kuipongeza Tanzania kwa kuchangia ulinzi wa amani duniani na kwamba nchi hiyo inaunga mkono jitihada zote zinazofanywa na Tanzania katika kuhakikisha Kanda ya Maziwa Makuu inakuwa na amani na utulivu.