Skip to main content
News and Events

TANZANIA KUWA MWENYEJI WA KONGAMANO NA MAONESHO YA 11 YA PETROLI AFRIKA MASHARIKI

Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) umeipitisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mwenyeji wa Kongamano na Maonesho ya 11 ya Petroli Afrika Mashariki yanayotarajiwa kufanyika tarehe 7 hadi 9 Machi 2025.

Mbali na hayo mkutano huo umepitisha bajeti ya kiasi cha Dola za Marekani 1,842,467 kwa ajili ya maandalizi ya kongamano na maonesho hayo.

Kongamano hilo litakalohusisha wadau kutoka serikalini na sekta binafsi linalenga kubadilishana taarifa kuhusu hali ya maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi asilia miongoni mwa Nchi Wanachama wa Jumuiya, na kutangaza fursa zilizopo katika ukanda kwenye sekta hiyo, hususan fursa za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia.  

Katika hatua nyingine mkutano huo umetoa mapendekezo kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuongeza kasi na bajeti ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati katika ngazi ya Taifa na Jumuiya itakayoimarisha upatikanaji wa nishati ya kutosha, bei nafuu, endelevu na salama kwa maendeleo ya Jumuiya na watu wake.

Aidha, katika mkutano huo ulioongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Shaibu Hassan Kaduara ambaye pia ni Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Zanzibar umependekeza kuwepo kwa mkakati wa pamoja wa Jumuiya wa kukabiliana na kuzuia uharibifu wa miundombinu mbalimbali ya nishati ikiwemo ya usambazaji na usafirishaji.

Akifungua mkutano huo Waziri Kaduara ameeleza kuwa Jumuiya itaweza kuchochea ongezo la uwekezaji, ajira na ukuaji maradufu wa uchumi na biashara endapo, pamoja na masuala mengine kutakuwepo na upatikana wa nishati ya uhakika na salama. 

“Sekta ya Nishati ina umuhimu wa kipekee katika kufanikisha  maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Jumuiya. Hivyo umuhimu wa  upatikanaji wa nishati ya uhakika, salama na gharama nafuu ni jambo la lazima na sio la hiyari kwani ni kichocheo cha kuvutia uwekezaji na kufanya bidhaa na huduma zinazozalishwa kuwa shindani katika soko la ndani na kimataifa”.  Alieleza Waziri Kaduara

Vilevile Mhe. Kaduara alitumia fursa ya mkutano huo kutoa mwaliko kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuja nchini, kushuhudia na kushiriki katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa umeme wa Maji wa Bwawa la Julius Nyerere, unaotarajia kuzalisha Megawatts 2115 utakaofanyika tarehe 25 Februari 2024.

Mkutano huo wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki, uliofanyika kwa siku tatu kuanzia 12-14 Februari 2024 katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha, ulitanguliwa na Mkutano wa Wataalam na Makatibu Wakuu.

  • Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Zanzibar Mhe. Shaibu Hassan Kaduara ambaye akifurahia jambo wakati akiongoza Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha
  • Viongozi wanaosimamia sekta ya nishati kutoka Nchi Wanachama wa EAC wakisaini (walioketi) taarifa ya Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha tarehe 14 Februari 2024. Waliosimama ni Watendaji mbalimbali kutoka nchi wanachama wakishuhudia zoezi hilo.
  • Meza Kuu wakiongoza Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha.
  • Sehemu ya ujumbe wa Tanzania wakifuatilia Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha