Skip to main content
News and Events

Tanzania , Brazil Zajizatiti Kuimarisha Diplomasia ya Uchumi

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, amekutana na kuzungumza na Balozi wa Brazil nchini Mheshimiwa Gustavo Martins Nogueira, katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Viongozi hao wamekutana kwa lengo la kuangalia namna ya kuendelea kuimarisha ushirikiano katika nyanja za diplomasia ili kuleta maendeleo kwa pande zote mbili.

Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Shelukindo amesema mafanikio makubwa yaliyopatikana Brazil katika maendeleo ya jamii, kilimo endelevu, nishati mbadala, na utoaji wa huduma za afya na michezo, yameitia moyo Tanzania na kutambua fursa zaidi za kuimarisha ushirikiano.

Balozi Shelukindo amesema eneo la utengenezaji na uunganishaji wa magari hususani mabasi ya kisasa yanayotumia umeme au gesi, ni eneo muhimu ambalo Tanzania inakusudia kupanua wigo na ushirikiano ili kukuza usafirishaji endelevu kwa manufaa wananchi wake.

“Kampuni kubwa kama Marcopolo ni muhimu ikaja Tanzania ili kuchochea kasi ya nchi yetu katika utengenezaji na uunganishaji wa magari, hususani mabasi ya kisasa, hatua itakayowezesha mataifa haya mawili kukuza biashara na uwekezaji.” Alifafanua Balozi Shelukindo.

Aidha, katika harakati za kukuza diplomasia ya michezo na utamaduni, Balozi Shelukindo amesema Tanzania na Brazil hazina budi kuanzisha miradi ya uwekezaji ikiwemo ujenzi wa vyuo vya kisasa vya michezo, ambapo wanamichezo maarufu wa Brazil kama Ronaldo Nazário na wengineo, wanaweza kushiriki kama wakufunzi, hivyo kuchangia maendeleo ya sekta hiyo, kupitia mchezo wa soka.

Naye Balozi wa Brazil nchini, Mheshimiwa Gustavo Martins Nogueira, ameipongeza Tanzania kwa ushirikiano imara na nchi yake na kuahidi kuwa Brazil itaendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania katika maeneo ya ulinzi na usalama, mafunzo ya kijeshi, udhibiti wa shughuli haramu katika ukanda wa bahari, uendelezaji wa kilimo hasa zao la pamba, na uwekezaji katika sekta ya mifugo, hususani nyama.