Skip to main content
News and Events

RAIS SAMIA AWATAKA MABALOZI KUENDANA NA MABADILIKO YA DUNIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka mabalozi wa Tanzania Nje ya Nchi kuendana na mabadiliko ya dunia katika utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi ili ilete tija zaidi kwa Taifa.

Rais Samia ametoa maelekezo hayo wakati akifungua rasmi Mkutano wa Saba wa Mabalozi unaoendelea Zanzibar.

Amesema ili kuhakikisha Tanzania inanufaika kiuchumi kisiasa na kijamii katika kipindi hiki ambacho dunia inapitia mabadiliko na changamoto mbalimbali, ni wajibu kwa Wizara pia kubadilisha mbinu, mikakati na vipaumbele katika utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje ili kufikia malengo kusudiwa. 

Mhe. Rais ameongeza kusema kuwa yapo masuala mapya yanayoendelea duniani ambayo kwa kiasi kikubwa yanaiathiri Tanzania kiuchumi, kisiasa, kijamii na hata kidiplomasia kwa ujumla wake na ambayo Sera ya Mambo ya Nje inapaswa kuyazingatia ili kwenda sambamba na mabadiliko hayo.

Amesema Sera ya Mambo ya Nje ya miaka 20 iliyopita inatakiwa kutathminiwa ili pamoja na mambo mengine iweze kutoa majibu katika kushughulikia changamoto hizo mpya za dunia ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, changamoto za afya, Mapinduzi ya Nne ya Viwanda, mabadiliko ya mwelekeo wa uchumi wa dunia, uhalifu wa Kimataifa, kutanuka kwa matumizi ya lugha ya kiswahili na namna ya kuwashirikisha Dispora katika kuchangia maendeleo ya nchi.

“Mabalozi naomba tuongeze uwajibikaji kwa kushirikiana na wadau wote muhimu wa Serikali na Sekta binafsi ili kuhakikisha Diplomasia ya Tanzania inakwenda na wakati na ufanisi,” alisema Rais Samia. 

Rais Samia ameongeza kuwa Sera ya Mambo ya Nje hutafsiri sera za ndani katika mawanda mapana ya sera za kimataifa kwa maslahi ya Taifa, ambapo Sera hiyo hutekelezwa na wadau wengi chini ya uratibu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. 

“Hili ni jukumu lenu mabalozi kwenye maeneo yenu ya uwakilishi, kuchukua sera zetu za ndani na kuzianisha na sera za nje na kupanga namna ya kutekeleza kila mmoja kwa wakati wake kwa maslahi mapana ya taifa letu,” alisema Rais Samia 

"Sote ni mashahidi wa hali ya uchumi wa dunia umebadilika, tena kwa kasi kubwa katika muongo mmoja uliopita, Sera yetu ya Mambo ya Nje imezinduliwa mwaka 2001. Katika kipindi hiki, kuna mambo mengi yamebadilika ndani ya dunia nasi ni vyema kukaa kwenye mkutano wa aina hii kuiangalia sera yetu yenye miaka 20 je bado ina mashiko kwenye mabadiliko ya dunia ya sasa hivi? Lakini je kwa kipindi cha miaka minne iliyopita ambayo hatukukaa mambo yepi yametupita na yapi yanatufaa kuendelea nayo,” amesema Rais Samia 

Mambo mengine ni kubadilika kwa mwelekeo wa uchumi wa dunia ambapo ukuaji wa uchumi ukiwemo uzalishaji, biashara na uvumbuzi vimehamia katika bara la Asia ambalo linazalisha asilimia 40 ya pato la dunia na kuwataka Mabalozi kujadili kuhusu namna ya kunufaika na fursa hiyo.

Pia ameongeza kusema kuongezeka kwa kasi ya utengamano katika bara ya Afrika ikiwemo kutanuka kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka wanachama watano hadi saba baada ya kuongezeka kwa Sudani Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Kadhalika, kuanza kutekelezwa kwa itifaki ya Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) pamoja na kuibuka kwa mahitaji mapya ya ndani ikiwemo kukua kwa uchumi wa buluu na lenyewe linahitaji kuwekewa mikakati. Jingine ni kuongezeka kwa matumizi ya lugha ya Kiswahili duniani, ambapo jukumu hilo pia ni lenu mabalozi.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) amesema kuwa Mkutano huo ulioanza tarehe 14 Novemba, 2022 umetoa fursa kwa Mabalozi na Konseli Wakuu kujadiliana na Viongozi, Watendaji na wadau mbalimbali toka sekta ya Umma na Sekta Binafsi kuhusu masuala mahsusi, yanayolenga kuboresha ushirikiano, na uwakilishi wao. 

“Wizara itaendelea kuzingatia maagizo yako Mhe. Rais, kuwa pande zote mbili za Muungano zinashirikishwa kikamilifu katika ziara za viongozi wetu wakuu, ziara za mawaziri, shughuli za kimataifa na kikanda, na katika kutafuta fursa za kuendeleza uchumi katika sekta mbalimbali,” alisema Dkt. Tax.

Dkt. Tax ameongeza kuwa Wizara itaendelea kuratibu kwa makini ili Tanzania iweze kuzitumia fursa zote kwa tija na maslahi ya Taifa, kwa kushirikiana na wadau kutoka sekta ya umma na binafsi.

Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) amesema kuwa wamepokea maelekezo ya viongozi wote wakuu wa Tanzania na Zanzibar na kuahidi kutekeleza diplomasia ya uchumi kwa maslahi mapana ya pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

  • Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiwatambulisha Mabalozi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati wa Mkutano wa mabalozi wa Tanzania Nje ya Nchi
  • Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wizara wakati wa mkutano kati ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na Mabalozi wa Tanzania
  • Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine akitoa neno la utangulizi wakati wa mkutano kati ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na Mabalozi
  • Meza kuu ikiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika picha ya pamoja na uongozi wa Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
  • Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga ambaye pia alikuwa mshereheshaji akizungumza wakati wa mkutano wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na Mabalozi
  • Sehemu ya Mabalozi wakifuatilia mkutano kati yao na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan uliofanyika Zanzibar 19 Novemba 2022
  • Meza kuu ikiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika picha ya pamoja