Skip to main content
News and Events

MTANZANIA ANAYEISHI NCHINI CANADA AONESHA NIA YA KUWEKEZA NCHINI KATIKA SEKTA YA MIUNDOMBINU YA BARA

Mtanzania anayeishi nchini Canada Bw. Joseph Katallah ameonesha nia ya kuja kuwekeza nchini katika sekta ya miundombinu kwa kushirikiana na kampuni ya Geopolymer Solutions LLC ya nchini Marekani hususan kwenye ujenzi wa barabara za lami kwa kutumia teknolojia mpya iliyogunduliwa na kampuni hiyo.

Wawekezaji hao wanaoratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wapo nchini kwa ziara ya wiki moja ambapo wanatumia fursa hiyo kukutana na wataalamu wa sekta ya barabara kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini Tanzania - TARURA, Wakala wa Barabara Tanzania  - TANROADS, na Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Lengo la ziara ya wawekezaji hao pamoja na mambo mengine ni kuitangaza teknolojia mpya ya utengenezaji wa barabara za lami zisizotumia saruji ya kiwandani na badala yake zitatumia udongo mwekundu ambao pia unapatikana nchini.

Wawekezaji hao wameeleza kuwa Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kupewa kipaumbele katika uwekezaji wa teknolojia hiyo kufuatia uwepo wa rasilimali za kutosha hapa nchini zitakazowezesha matumizi ya teknolojia hiyo yenye gharama nafuu na rafiki kwa mazingira ili iweze kutumika kuchochea maendeleo chanya kwa Taifa.

Wakati huo huo, wataalamu kutoka sekta ya barabara wameeleza kuwa ni vema uwekezaji wa aina hiyo ukafuata taratibu zilizowekwa katika mfumo wa Serikali na kuruhusu kufanyika kwa tafiti inayopimika ili kujiridhisha na ufanisi wake katika ardhi na hali ya hewa ya Tanzania.

Vilevile, wakaeleza umuhimu wa teknolojia hiyo kufanyiwa majaribio katika maeneo korofi kufuatia wawekezaji hao kueleza ufanisi wa teknolojia hiyo katika maeneo mengi korofi ambayo kampuni zenye teknolojia nyingine zimeshindwa kukidhi na kudhibiti changamoto hiyo. 

Hivyo, kikao hicho kiliazimia wawekezaji hao wakutane na wataalamu wanaoshughulikia viwango vya ubora wa barabara nchini ili kujihakikishia ubora na ufanisi wa teknolijia hiyo mpya kabla ya kufikia hatua ya kukubaliana na uwekezaji huo.  Pia uhakiki huo utasaidia kufahamu unafuu wa gharama, uokoaji wa muda, sambamba na upekee na uwezo wa teknolojia hiyo mpya ukilinganishwa na teknolojia inayotumika sasa.

Kampuni ya Geopolymer Solutions LLC inauzoefu wa kufanya kazi katika nchi za Canada, Marekani na Uingereza.  Kwa upande wa nchi za Bara la Afrika, pamoja na kutoa kipaumbele kwa Tanzania pia nchi ya Ghana imeonesha kuhitaji kujifunza teknolojia hiyo mpya.

  • Wajumbe wengine kutoka sekta za Ujenzi wakifuatilia kikao hicho.
  • Bi. Mwakawago akizungumza na Mhandisi John ngowi na Dkt. Philemon Msomba kutoka Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TATURA) mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho.