Skip to main content
News and Events

MHE. RAIS SAMIA AFUNGUA RASMI MKUTANO WA WAKUU WA NCHI ZA AFRIKA KUHUSU RASILIMALI WATU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa rai kwa nchi za Afrika kuwekeza zaidi katika kuboresha afya, elimu na lishe kwa watu wake ili kutengeneza rasilimali watu inayoweza kuchangia maendeleo na ukuaji wa uchumi barani Afrika. 

Rai hiyo ameitoa jijini Dar es Salaam leo tarehe 26 Julai 2023 wakati akifungua rasmi Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Rasilimali Watu uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere.

Amesema Mkutano huu umetoa fursa kwa nchi za Afrika kujadili na kupanga mikakati mipya ya namna ya kutumia Rasilimali Watu ambayo Afrika imejaliwa kuwa nayo kama nyenzo muhimu katika kuchangia maendeleo na mafanikio ya Bara la Afrika. 

Ameongeza kusema kwa upande wa Tanzania tayari mikakati mbalimbali imewekwa ya kuendeleza Rasilmali Watu ikiwemo kutenga fedha kwa ajili ya kuongeza afua za lishe na huduma za afya ya mama na mtoto ambapo amesema ameingia mkataba na Wakuu wa Mikoa kuhakikisha wanasimamia suala hili katika mikoa yao.

 Amesema ifikapo mwaka 2050 Afrika itakuwa na asilimia 42 ya vijana duniani kote hivyo uwekezaji kwenye rasilimali watu yenye tija unahitajika ili kuwa na hatima nzuri. Amesema jitihada zaidi zinahitajika ili kuepuka kuzalisha vijana wasio na ujuzi, wasio ajirika na vijana wenye kujiingiza kwenye vitendo viovu vya kihalifu na uvunjifu wa amani. 

Ameongeza kusema uwekezaji kwenye rasilimali watu unaanza tangu mtoto anapozaliwa kwa kumpatia lishe bora na chanjo stahiki ili kuondoa udumavu ambao husababisha upungufu wa uelewa na uwezo wa kusoma vizuri kwa watoto. Pia amesisitiza kuwekeza katika elimu ya awali ambayo ni msingi wa kuwaandaa watoto kimwili, kiakili, kihisia na kiubunifu.

Kadhalika ameeleza kuwa Tanzania inaendelea kuboresha utoaji huduma za jamii na kufanya maboresho ya miundombinu kama madarasa, vituo vya afya, kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa sekta ya elimu na afya na kutekeleza mpango wa elimu bure kwa shule za msingi hadi sekondari.

wali akizungumza, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa kuridhia Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano huo muhimu ambao amesema umehudhuriwa na zaidi ya Washiriki 2,500. Pia ameipongeza na kuishukuru Benki ya Dunia kwa kuandaa mkutano huo kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania.

Amesema Mkutano huo ni jukwaa kwa nchi za Afrika kupanga mikakati bora zaidi ya kuendeleza rasilimali watu kwa maendeleo endelevu ya Bara la Afrika.

Naye Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwakwa amesma Benki hiyo itaendelea kushirikiana na kuunga mkono jitihada mbalimbali zinazofanywa na Nchi za Afrika katika kuendeleza rasilimali watu ili hatimaye kuwa na maendeleo ya kijamii na kiuchumi. 

Mkutano huo ambao umehudhuriwa na Wakuu wa Nchi kutoka Nchi sita za Kenya, Madagascar, Sao Tome na Principe, Sierra Leone, Malawi na Msumbiji na wadau mbalimbali kutoka sekta binafsi naza umma umemalizika kwa kupitishwa kwa Azimio la Dar es Salaam ambalo limeainisha mikakati ya kuboresha maendeleo ya rasilimali watu barani Afrika.

  • Mhe. Rais Samia akihutubia mkutano
  • Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akitoa neno la utangulizi wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Rasilimali Watu kabla ya kumkaribisha Mhe. Rais Samia kufungua rasmi mkutano huo.
  • Mhe. Rais Dkt. Samia (wa nne kushoto) akiwa na Marais walioshiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Rasilimali Watu. Kutoka kushoto ni Mhe. Rais Ruto, Mhe. Rais Chakwera, Mhe. Rais Nyusi, Mhe. Rais Andry Rajoelina wa Madagascar, Mhe. Rais Carlos Vila Nova wa Sao Tome na Principe na Mhe. Rais Julius Maada Bio wa Sierra Leone
  • Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwakwa akizungumza wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Rasilimali Watu
  • Marais kutoka Nchi za Afrika ni miongoni mwa viongozi waliohudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Rasilimali Watu. Kutoka kushoto ni Rais wa Kenya, Mhe. William Ruto, Rais wa Malawi, Mhe. Lazarus Chakwera na Rais wa Msumbiji, Mhe. Filipe Nyusi