Makamu wa Rais Asisitiza Utekelezaji wa Mipango ya Pamoja ya Maendeleo Afrika
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amezitaka nchi za Afrika kuongeza kasi ya kutekelezaji wa makubaliano, sera na mikakati ya pamoja ya maendeleo ili kutumia kikamilifu fursa na rasilimali zilizopo barani humo kwa manufaa ya wananchi.
Mkamu wa Rais Mhe. Ndejembi alitoa rai hiyo Oktoba 3, 2026, wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika majadiliano ya ngazi ya juu ya Alamein Africa Business Forum yaliyofanyika jijini El- Alamein, Misri.
Alisema kuwa Afrika ina mipango na maono mazuri ya maendeleo, isipokuwa inakabiliwa changamoto katika utekelezaji wa makubaliano na mipango hiyo ili ilete matokeo yanayoonekana kwa wananchi.
Vilevile, Makamu wa Rais Mhe. Ndejembi alisisitiza kuwa Afrika inahitaji kujenga uchumi unaostahimili misukosuko ya nje kwa kuongeza uzalishaji, kuimarisha biashara ya ndani ya bara, pamoja na kuwekeza katika nishati, miundombinu, viwanda na teknolojia.
Akieleza hatua zinazochukuliwa na Tanzania, Makamu wa Rais alitaja uwekezaji katika sekta ya nishati, ukiwemo Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115, na kutekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo imeweka nishati na miundombinu miongoni mwa maeneo muhimu ya kuchochea uzalishaji, viwanda na mageuzi ya kiuchumi.
Mhe. Ndejembi pia alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, uwekezaji unaovuka mipaka na kuunganisha uchumi wa nchi za Afrika ili kuongeza uzalishaji, ajira, biashara na thamani ya rasilimali zinazozalishwa barani.
Aidha, ameeleza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi nyingine za Afrika, hususan Afrika Mashariki, katika kutekeleza miradi ya kimkakati ya miundombinu, ikiwemo reli, nishati, mafuta na bandari, kwa lengo la kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kuchochea biashara na mtangamano wa kikanda.
Jukwaa hilo lilifunguliwa na Rais wa Misri, Mhe. Abdel Fattah El-Sisi, na Rais wa Burundi na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Mhe. Évariste Ndayishimiye, likiwakutanisha viongozi wa Serikali, taasisi za fedha na sekta binafsi kutoka Afrika na maeneo mengine duniani.
Jukwaa la Biashara la Alamein Afrika (Alamein Afrika Business Forum) lililofanyika kwa mara ya kwanza linalenga kuunganisha Serikali, sekta binafsi, taasisi za fedha na wadau wengine wa maendeleo ili kuimarisha biashara, uwekezaji, ubia wa sekta ya umma na binafsi na utekelezaji wa Agenda 2063.