Skip to main content
News and Events

MAKAMU WA RAIS AMUWAKILISHA RAIS SAMIA KWENYE HAFLA YA UWEKAJI JIWE LA MSINGI LA UKARABATI MKUBWA WA RELI YA TAZARA.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, leo Novemba 20, 2025 amemuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la Uzinduzi wa Ukarabati Mkubwa wa Reli ya TAZARA iliyofanyika jijini Lusaka nchini Zambia.

Mheshimiwa Nchimbi amesema ukarabati wa reli ya TAZARA utaimarisha Ukanda wa Kati na Kusini pamoja na kuchochea biashara katika mataifa kadhaa yakiwemo Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Bara la Afrika kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kukuza kilimo, madini, viwanda, utalii na kutengeza ajira zaidi kwa wananchi wa ukanda huo.

Mheshimiwa Nchimbi amesema wakati reli ya TAZARA inaimarishwa, Tanzania inafanya maboresho ya kisasa ya bandari ikiwemo dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam kwa magati mapya, kuboresha ufanisi, na kuhakikisha muunganiko mzuri wa Reli ya Umeme ya Kisasa (SGR) na TAZARA. Ameongeza kwamba, Tanzania itaendelea kuboresha bandari za Tanga, Mtwara na Bagamoyo ili kuhakikisha kwamba kunakuwa na ubora wa kimataifa wa usafirishaji kwa nchi za Zambia, SADC na Afrika kwa ujumla.

Halikadhalika, Makamu wa Rais amesema ukarabati huo unakuja wakati China inaibuka kama mdau muhimu wa ukuaji wa uchumi kimataifa chini ya mpango wake wa 15 wa Miaka Mitano. Amesema hali hiyo inaiweka China kama mshirika muhimu wa maendeleo.

Makamu wa Rais amesema historia inafundisha ukweli wenye nguvu kwamba, Tanzania, Zambia na China zinaposimama pamoja, hakuna changamoto iliyo kubwa. Amesema ikiwa waasisi wa mataifa hayo, waliweza kujenga Reli ya Uhuru, kwa sasa ikizingatiwa mataifa na uwezo yaliyonayo yataweza kukarabati Reli ya TAZARA na kuifanya kuwa mfano wa ushirikiano wa karne ya 21.