Skip to main content
News and Events

MAKAMU WA KWANZA WA RAIS ZANZIBAR AFUNGUA KONGAMANO LA PILI LA UWEKEZAJI KATI YA TANZANIA NA ITALIA

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman amesema Serikali ya Zanzibar inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuwawezesha Wawekezaji wenye tija kuwekeza katika sekta  mbalimbali  ikiwemo sekta ya Uchumi wa Bluu.


Mhe. Othman ametoa kauli hiyo wakati akifungua rasmi Kongamano la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika Zanzibar tarehe 28 Septemba, 2022 na kuwashirikisha wadau mbalimbali wa masuala ya biashara na uwekezaji kutoka Tanzania na Italia.


Mhe. Othman ambaye alimwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwenye kongamano hilo amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imefungua milango kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali na kwamba inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara kwa kuzifanyia maboresho sheria na kanuni mbalimbali za uwekezaji.

Kadhalika alisema maboresho hayo yanakwenda sambamba na yale ya sekta ya utoaji huduma kama vile za viza, vibali vya kazi na ukaazi pamoja na  kuboresha mawasiliano kupitia mifumo ya kidigitali ambapo Serikali hiyo inatarajia hivi karibuni kuzindua  mfumo wa uombaji viza kwa njia ya mtandao.


"Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuifanya Zanzibar kuwa miongoni mwa maeneo bora ya uwekezaji duniani. Uwekezaji una manufaa makubwa ya kiuchumi kwa nchi ikiwa ni pamoja na kukuza pato la taifa pamoja na kutenegeneza ajira kwa vijana na wanawake" alisema Mhe. Othman.


Mhe. Othman ameeleza kuwa, katika kipindi cha miaka miwili kuanzia mwezi Novemba 2020 hadi wakati wa kongamano hilo Zanzibar imesajili miradi ya uwekezaji 196 yenye thamani ya dola za marekani bilioni 1.4 ambapo miradi hiyo inatarajiwa  kutengeneza ajira zipatazo 9,000. Hivyo alihimiza washiriki kutumia  Kongamano hilo kama  chachu ya kuhamasisha wawekezaji wengi zaidi kuja nchini.  

“Kongamano hili liwe chachu ya kuvutia na kuhamasisha wawekezaji zaidi kuja Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Naendelea kutoa wito kwa wawekezaji kutoka Italia na duniani kote kuchangamkia fursa lukuki za uwekezaji tulizonazo. Namaliza kwa kusema Wekeza Zanzibar, Wekeza sasa” alisisitiza Mhe. Othman


Awali akizungumza wakati wa kongamano hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mhe. Mudrick Soraga amepongeza jitihada zinazofanywa na Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo na Balozi mwenzake wa Italia hapa nchini, Mhe. Marco Lombardi za kuandaa kongamano hilo kwa mara ya pili ikiwa ni mchango wao wa kuhakikisha nchi hizi mbili zinanufaika kupitia ushirikiano mzuri uliopo.

Pia aliwataka washiriki wote kutumia kongamano hilo kama fursa ya kubadilishana  mawazo na uzoefu miongoni mwao ili kuendelea kuboresha sekta ya biashara na uwekezaji  nchini. 

 Mhe. Soraga  pia alitumia fursa hiyo kuainisha fursa za kipaumbele za uwekezaji Zanzibar kuwa ni pamoja na Sekta ya Uchumi wa  Bluu, Kilimo, Usindikaji wa mazao ya kilimo, Utalii, ufugaji wa samaki, utalii unaozingatia utunzaji wa mazingira, miundombinu, nishati na uwekezaji katika mali zisizohamishika kama majengo.

Wakati wa Kongamano hilo mada mbalimbali ziliwasilishwa na kujadiliwa ikiwemo Maendeleo ya Miundombinu, Uchumi wa Bluu na Kilimobiashara na Kilimo cha Kisasa cha kutumia mashine na mitambo. Kongamano hilo ambalo limewashrikisha wadau kutoka sekta mbalimbali za biashara na uwekezaji wa hapa nchini na kutoka Italia litahitimishwa rasmi tarehe 30 Septemba 2022 jijini Dar es Salaam.

  • Sehemu ya Mabalozi na wageni waalikwa wakifuatilia hotuba ya Mhe Soraga
  • Sehemu ya Washiriki wa Kongamano wakifuatilia hotuba ya ufunguzi kutoka kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman
  • Mhe. Makamu wa Kwanza wa Rais akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (kushoto) na Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi (katikati)
  • Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mhe. Mudrick Soraga nae akizungumza wakati wa Kongamano hilo
  • Mkurugezni Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) akifafanunua fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo Zanzibar