Skip to main content
News and Events

FILAMU YA “THE ROYAL TOUR” ILIYOTAFSIRIWA KIJAPAN YAZINDULIWA JAPAN

Tanzania imetumia Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Japan (Japan Tourism Expo) yanayofanyika nchini humo kuanzia tarehe 22 – 25 Septemba 2022 kuzindua filamu ya “The Royal Tour” iliyotafsiriwa kwa lugha ya Kijapan.

Katika hotuba yake wakati wa ufunguzi wa maoenesho hayo uliofanyika jana tarehe 22 Septemba 2022, Balozi wa Tanzania nchini Japan, Mhe. Baraka Luvanda aliwasihi washiriki wa maonesho hayo kuiangalia filamu ya “The Royal Tour” ambayo inavionesha vivutio vya Tanzania kama vile hifadhi za taifa za wanayamapori, milima na fukwe za kuvutia kwa ufasaha.

Balozi Luvanda aliwaeleza kuwa tukio hilo la uzinduzi wa filamu limefanyika katika kipindi kizuri ambapo dunia inaanza kufunguka kutokana na masharti ya kusafiri baina ya nchi kupunguzwa, kufuatia kupungua kwa mambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Corona duniani.

“Ni matumaini yangu kuwa washiriki wa maonesho haya na wageni wengine, mtapanga safari za kutembelea Tanzania kujionea wenyewe vivutio vya utalii mnavyovishuhudia katika filamu hii na kwenye banda la Tanzania lililopo kwenye Maonesho haya”, Balozi Luvanda alisisitiza. 

Tanzania imejipanga kutangaza vivutio vya utalii kwa kutumia majukwaa mbalimbali yakiwemo kama hayo ya Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Japan ambayo yanashirikisha wadau wengi wa utalii kutoka duniani kote. 

Wadau wa Tanzania wanaoshiriki maonesho hayo ni pamoja na; Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS). 

  • Sehemu ya Filamu ya "The Royal Tour" ikimuonesha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan alivyokuwa akiapa kushika wadhifa huo
  • Wageni wanaotembelea Banda la Tanzania katika Maonesho ya Kimataifa ya Utalii yanayoendelea nchini Japan wakiangalia Filamu ya "The Royal Tour"
  • Banda la Tanzania limependeza kweli kweli ambapo linavutia wageni wengi kulitembelea.