Skip to main content
News and Events
Press Release

DKT. KIKWETE AHIMIZA AMANI KATIKA NCHI ZA SADC

Imeelezwa kuwa amani na usalama ni maneno yenye dhana pana tofauti na watu wengi wanavyoelewa kuwa amani na usalama ni kuwa huru na migogoro inayotumia silaha.

Hayo yameelezwa Agosti 12, 2023 na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungani wa Tanzania, Mhe. Jakaya Nrisho Kikwete wakati anawasilisha mada kuhusu Amani na Usalama kama kigezo cha msingi cha kufikia maendeleo ya kweli Kusini mwa Afrika.

Mhe. Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jopo la Wazee wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) aliwasilisha mada hiyo kwenye Chuo cha Diplomasia cha Angola ikiwa ni moja ya matukio ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC ulioanza tarehe 08 Agosti 2023 kwa ngazi ya maafisa waandamizi na utahitimishwa na Mkutano wa Marais utakaofanyika tarehe 17 Agosti 2023.

“Amani na Usalama ni dhana pana inayojumuisha mambo mengi kama vile elimu, afya na ustawi wa jamii”, Mhe. Kikwete alisema.

Alieleza kuwa amani na usalama ni msingi wa maendeleo Kusini mwa Afrika na itakapokosekana mahali popote pale, watu wasitarajie kupata maendeleo. Alitoa mfano wa nchi zilizokuwa na migogoro ya kisiasa kwa muda mrefu kama Angola na Msumbiji namna zilivyoathirika kiuchumi hadi hapo ufumbuzi ulipopatikana. Alisema, utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani na mazingira tulivu yaliyopo hivi sasa, imeshuhudiwa mataifa mengi ya kusini mwa Afrika yanapiga hatua za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Aliongeza kuwa taifa lisilokuwa na amani haliwezi kufanya biashara; haliwezi kuvutia uwekezaji kutoka nje na hata ndani ya nchi; haliwezi kujenga miundombinu kama ya Barabara, shule na vituo vya afya kwa sababu fedha zote ambazo Serikali inazipata, zinatumika kununua silaha kwa ajili ya kujilinda. 

Alihitimisha mada yake kwa kusisitiza umuhimu wa nchi za SADC zishirikiane kuhamasisha amani katika nchi zao. Amani itaziwezesha Serikali za nchi hizo kujiamini na hatimaye kuwa na utawala bora, utawala wa sheria na kutoa haki kwa watu wote.

Viongozi wengine mashuhuri walioungana na Rais Kikwete kuwasilisha mada katika Mhadhara huo wa Umma ni Waziri Mkuu Mstaafu wa Msumbiji, Mhe. Luisa Diogo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Zamani wa Angola, Mhe. Balozi Joao Bernardo de Miranda ambao mada zao zilihusu miundombinu inayohitajika kuunganisha nchi za SADC na hali ya sasa ya dunia na athari zake kwa nchi za SADC.