Skip to main content
News and Events

Balozi Mteule wa Jamhuri ya Kazakhstan awasilisha Nakala za Hati za Utambulisho

Balozi Mteule wa Jamhuri ya Kazakhstan mwenye makazi yake mjini Pretoria, nchini Afrika Kusini, Mhe. Yerkin Akhinzhanov amewasilisha Nakala za Hati za Utambulisho kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Dennis Londo (Mb).

Akipokea Nakala za Hati hizo kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, katika Ofisi ndogo za Wizara, jijini Dar es Salaaam Mhe. Londo ampongeza Mhe. Akhinzhanov kwa kuaminiwa na kuteuliwa kuiwakilisha nchi yake hapa nchini na kuahidi kuwa Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, itampatia ushirikiano wakati wote ili kumwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Mhe. Londo amesema Serikali ya Tanzania na Jamhuri ya Kazakhstan zimeendelea kukuza ushirikiano katika Nyanja ya biashara na uwekezaji, hususani katika sekta za uchimbaji madini ya Uranium na mafuta ya Petroli pamoja kubadilishana uzoefu katika tamaduni za mataifa hayo; hatua ambayo imewezesha kuimarisha uhusiano wa uwili kati ya nchi hizo kwa manufaa ya wananchi wa pande zote.

Naye Balozi Mteule wa Jamhuri ya Kazakhstan Mhe. Akhinzhanov ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa jitihada zake za kuimarisha ushirikiano na nchi yake kwani itasaidia kufungua milango ya biashara, Uchumi, Sekta ya Fedha ya Kimataifa na hatimaye kukuza uhusiano ya kidiplomasia.