Skip to main content
News and Events

ANZANIA YAJIVUNIA MAFANIKIO WAKATI WA UENYEKITI WA SADC

ANZANIA YAJIVUNIA MAFANIKIO WAKATI WA UENYEKITI WA SADC 

Tanzania imejivunia mafanikio yaliyopatikana wakati ikiwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Mafanikio hayo yameelezewa katika Mkutano wa 40 wa Baraza la Mawaziri na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi ulifanyika kwa njia ya mtandao jijini Dar es Salaam. 

Kupitia mkutano huo, Prof. Kabudi  amekabidhi uenyekiti wa Baraza la Mawaziri kwa Balozi wa Msumbiji nchini, Mhe. Monica P. Clemente kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Msumbiji Mhe. Verónica Nataniel Macamo Dlhovo   

Prof. Kabudi amesema pamoja na janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu (COVID 19) jumuiya ya SADC imeendelea kufanya kazi zake, mikutano yake chini ya uongozi wa Tanzania kwa ufanisi wa hali ya juu kwa kupitia njia ya mtandao (video conference)

"Nasema ni mafanikio makubwa kwa sababu Jumuiya nyingine za kikanda zimeshindwa kufanya hivyo, sisi ndiyo jumuiya pekee iliyoanza utaratibu huu wa aina hii ya mikutano kwa sababu kwetu tuliona COVID 19 ni changamoto ambayo haiwezi kutuzuia kufanya shughuli zetu,". Amesema Prof. Kabudi

Prof. Kabudi ameongeza kuwa mbali na kupambana a janga la COVID 19, mafanikio mengine ni kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya nne katika jumuiya ya SADC, lugha nyingine ni Kiingereza, Kireno na Kifaransa.    

"Lugha ya Kiswahili kwa Tanzania ni lugha ya ukombozi wa Afrika, ndiyo lugha iliyotumika wakati wa kuwafundisha wapigania uhuru mbinu za kuwasiliana wakati wa ukombozi kwa mataifa ya Afrika," Amesema Prof. Kabudi.

Prof. Kabudi ameyataja mafanikio mengine yaliyopatikana wakati Tanzania ikiwa mwenyekiti wa SADC ni kusimamia na kukamilika kwa Mwongozo wa kusafirisha bidhaa na huduma kwa nchi wanachama katika kipindi cha (COVID-19). Mwongozo huo umelenga kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya virusi vya Corona na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na huduma mbambali baina ya nchi wanachama. 

Tanzania imewezesha agenda ya viwanda kutekelezwa ambapo wakati wa COVID 19 tumeweza kuongeza uwezo wetu wa kutengeneza dawa kwa kuwa mataifa makubwa duniani mara baada ya kuibuka kwa covid 19 walisitisha kuuza dawa katika nchi nyingine ili wazitumie dawa hizo ndani ya nchi zao.

"Tunaimani kuwa msingi uliowekwa wakati wa COVID 19 utaimarisha jitiada zetu za kuwa na uchumi wa viwanda, uchumi wa kati na uchumi wa juu. Na sisi imekuwa jambo la faraja kubwa kuingia katika uchumi wa kati kabla ya miaka mitano iliyokuwa imepangwa hapo awali," Amesema Prof. Kabudi.

"Chaguzi katika nchi za Malawi, Mauritius, Namibia zimefanyika kwa amani na utulivu. Ii imedhihirisha wazi kuwa demokrasia katika ukanda wetu inazidi kukua………haya yote ni mafanikio makubwa kwetu tukiwa mwenyekiti wa SADC," ameongeza Prof. Kabudi.

Nae Balozi wa Msumbiji nchini, Mhe. Monica Clemente aliyemuwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje Msumbiji, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi kubwa aliyofanya wakati wa Uenyekiti wake wa SADC. 

Amefanya mambo makubwa kabisa kwa nchi wanachama wa SADC na amekuwa kama Mwalimu kwa nchi nyingine kutokana na maendeleo yaliyopatikana wakati wa uongozi wake akiwa mwenyekiti wa SADC. 

"Sisi Msumbiji tunashukuru kwa kupokea Uenyekiti wa SADC na tunaahidi kujitahidi kadri ya uwezo wetu kuendeleza yale yote yaliyofanywa na Tanzania wakati akiwa Mwenyekiti, kwani Tanzania amekuwa mwalimu kwetu na nchi nyingine za SADC," amesema Balozi Monica. 

Mkutano wa 40 wa baraza la mawaziri umehudhuriwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango, Waziri wa Afya , Maendeleoya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa wakifuatilia mkutano kwa njia ya Mtandao (Video Comnference) 

Downloads File: