Skip to main content
News and Events

MAWIZIRI WA EAC KUKUTANA ARUSHA

MAWIZIRI WA EAC KUKUTANA ARUSHA

Mkutano wa 41 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unaendelea jijini Arusha katika ngazi ya maafisa waandamizi. Mkutano huo ulioanza  tarehe 22 Novemba 2021 utahitimishwa na Kikao cha Mawaziri wa Nchi za Jumuiya kitakachofanyika tarehe 29 Novemba 2021.

Tanzania ambayo ni mwanachama muasisi wa Jumuiya hiyo inashiriki kikamilifu katika mkutano huo ambapo Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Stephen P. Mbundi anaongoza ujumbe wa Tanzania katika ngazi ya maafisa waandamizi.

Maafisa waandamizi wanaandaa taarifa mbalimbali za utekelezaji wa shughuli za Mtangamano wa Afrika Mashariki ambazo zitawasilishwa kwenye ngazi ya Makatibu Wakuu na hatimaye ngazi ya Mawaziri kwa ajili ya kutolea maamuzi na maelekezo. 

Waheshimiwa Mawaziri pia watapokea na kupitia taarifa za utekelezaji wa vyombo na Taasisi za EAC, zikiwemo Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Ofisi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kamisheni ya Kiswahili ambayo Makao Makuu yake yapo Zanzibar na Kamisheni ya Sayansi na Teknolojia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Katika jitihada za Tanzania za kukuza lugha ya Kiswahili duniani, Waheshimiwa Mawaziri watapokea taarifa ya maendeleo ya mchakato wa kubadilisha sheria na taratibu za EAC ili kuwezesha kuanza rasmi matumizi ya  lugha ya Kiswahili pamoja na Kifaransa kama ilivyoelekezwa na Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki mwezi Februari 2021. Aidha, Waheshimiwa Mawaziri watapokea taarifa kuhusu mchakato wa uhakiki wa maombi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuwa mwanachama mpya wa EAC.

  • Mwenyekiti wa kikao kutoka Kenya akiendesha kikao cha maafisa waandamizi.
  • Baadhi ya ujumbe wa Tanzania ambao ni Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kiongozi wa ujumbe wa Tanzania katika kikao cha ngazi ya maafisa waandamizi, Balozi Stephen P. Mbundi, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Miundombimu ya Uchumi na Huduma za Jamii, Bw. Eliabi Chodota (mwenye peni) na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji, Bw. Benjamini Mwesiga (aliyesimama) wakijadili jambo wakati wa kikao cha maafisa waandamizi cha EAC.
  • Ujumbe a Tanzania ukifuatilia majadiliano kuhusu agenda mbalimbali za kikao cha maafisa waandamizi wa EAC.