Skip to main content
News and Events

MAJALIWA, DKT. KIKWETE WAONGOZA WAOMBOLEZAJI MAZISHI YA MEMBE

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete wameongoza mamia ya waombolezaji katika mazishi ya aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard Membe yaliyofanyika kijijini kweke Rondo, mkoani Lindi yaliyofanyika jana Jumanne tarehe 16 Mei 2023.

Akitoa salamu za Serikali kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Mhe. Majaliwa amesema kifo cha Bernard Membe kimewacha Watanzania na wana Lindi na simanzi, majonzi na huzuni isiyo na kifani.

"Kipekee Mhe. Rais Samia anawashukuru wananchi wote wa Lindi kwa utulivu mliouonesha wakati huu wa msiba wa Mzee Membe wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi kwa kuhakikisha shughuli ya mazishi inaenda vizuri kama ilivyokusudiwa, tunawashukuru na Mwenyezi Mungu aendelee kuwajaalia faraja na uvumilivu katika kipindi hiki cha majonzi mnachopitia," alisema Mhe. Waziri Mkuu.

Mhe. Majaliwa ameongeza kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango naye ameungana na Rais Samia kutoa pole kwa wana Lindi na wana Mtama na amewasihi kuendelea kuyaenzi mazuri yote aliyofanya enzi za uhai wake.

Marehemu Membe atakumbukwa kwa mengi hususani utumishi wake uliotukuka na hasa katika taasisi za Kimataifa alizohudumu wakati wa uhai wake ambapo pia ametumikia Watanzania katika nafasi mbalimbali na kuleta maendeleo. 

“Mchango wa marehemu Membe ni mkubwa hasa katika Jimbo la Mtama," alisema Mhe. Majaliwa.

Mhe. Waziri Mkuu aliongeza kuwa CCM imeelezea kazi nzuri aliyoifanya kwa nafasi mbalimbali alizoshika wakati wa utumishi wake, umahiri na weledi, alikuwa pia na siasa za kistaarabu hakika Chama kimempoteza kiongozi makini na hodari na utumishi uliotikuka, hakika alikuwa kiongozi wa kuigwa.

Kwa upande wake, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete alisema alifahamiana na Marehemu Membe muda mrefu na tangu wakati huo wamekuwa wakisaidiana mambo mengi katika kazi na nje ya kazi.

"Alikuwa msaada mkubwa kwangu wakati wote wa utumishi. Alifanya mambo makubwa na alileta medali za kimataifa kutokana na uchapa kazi wake wa kujitoa kwa moyo wake wote,"alisema Dkt. Kikwete.

Mhe. Dkt. Kikwete aliongeza kuwa Marehemu alikuwa mwanadiplomasia mahiri na aliyekuwa na mikakati mizuri iliyokuwa na mafanikio makubwa kwa taifa.......na alikuwa msomi mzuri lakini pia alikuwa mcha Mungu," alisisitiza Dkt. Kikwete.

Dkt. Kikwete aliongeza kuwa Marehemu Membe aliweka maslahi ya Tanzania mbele na hakutaka mchezo na maslahi ya taifa lake, alikuwa jasiri, hakika taifa limepoteza moja kati ya watu muhimu.

Akitoa salamu za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) alisema Marehemu Membe alitoa mchango mkubwa katika Wizara ya Mambo ya Nje na mchango huo utakumbukwa daima.

"Marehemu alikuwa mchapa kazi, mpenda watumishi wake, kiongozi mahiri na mwanadiplomasia nguli....na Kipindi cha uongozi wake, Serikali ilipata medali nyingi za Kimataifa kutokana na uchapa kazi wake," alisema Balozi Mbarouk.

Balozi Mbarouk aliongeza kuwa Marehemu Membe alikuwa ni Mwalimu na mfano bora wa kuigwa, hivyo kwa niaba ya watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki waliopo nchini na Nje ya nchi, Wizara inatoa pole kwa familia, Mungu awajalie uvumilivu wakati huu mgumu wa msiba.

Naye Katibu wa Itikadi na Uenezi wa (NEC), CCM Taifa, ndgu Sophia Mjema alisema Marehemu Membe aliyeshika nafasi mbalimbali kwenye Chama za Ubunge, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Mjumbe wa Sektrtariet ya Halmashauri Kuu ya Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa Ali fanya kazi y’a kukitetea Chama chake na daima watamkumbuka kwa hilo. 

"Membe alifanya kazi ya kutetea Chama chake CCM, alikuwa kiongozi makini na hodari, alikuwa mwana CCM kweli kweli, CCM itamkumbuka ndgu Membe kwa uanachama wake na uongozi wake mahiri...aliweza kukitetea Chama chake na kuiunganisha CCM na vyama rafiki katika Dunia," alisema ndugu. Mjema

Ndgu Mjema alisema kuwa CCM itaendelea kumkumbuka kwa kazi nzuri aliyoifanya.

Ibada ya mazishi ya Marehemu Membe ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainabu Telack, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Mstaafu Ahmed Abbas; Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Batilda Buriani; Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka.

Wengine ni Waziri wa TAMISEMI Mhe. Angela Kairuki, Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwan Kikwete, Mhe. William Lukuvi, Mbunge Isimani; Wakuu wa Wilaya mbalimbali na wakuu wa taasisi za Serikali na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa

  • Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) akitoa salamu za pole kwa familia na waombolezaji muda mfupi baada ya Ibada ya kumwombea Marehemu Bernard Membe iliyofanyika nyumbani kwake Rondo, Lindi
  • Sehemu ya Viongozi wakiweka mataji ya maua kwenye kaburi la Marehemu Bernard Membe
  • Waziri wa TAMISEMI Mhe. Anjela Kairuki (Kulia) na Balozi wa Tanzania nchini China Mhe. Mbelwa Kairuki (katika) wakiwasili nyumbani kwa Marehemu Bernard Membe Kijiji cha Rondo, Lindi kushiriki kwenye mazishi ya Mwanadiplomasia huyo ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
  • Mwili wa Marehemu Bernard Membe ukiwa kwenye ibada maalumu ya kumwombea muda mfupi kabla ya kupunzishwa kwenye nyumba yake ya milele.
  • Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) akiweka udongo kwenye kaburi la Marehemu Bernard Membe
  • Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (wa kwanza kushoto) akishiriki Ibada ya kumwombea Marehemu Bernard Membe
  • Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete akiwasili nyumbani kwa Marehemu Bernard Membe kijiji cha Rondo, Lindi ambapo aliongoza mamia ya waombolezaji kwenye mazishi ya Mwanadiplomasia huyo ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
  • Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) akisalimiana na baadhi ya waombolezaji alipowasili nyumbani kwa Marehemu Bernard Membe Rondo, Lindi kwenye mazishi ya Mwanadiplomasia huyo ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa