Skip to main content
News and Events
Press Release

INDIA, JAPAN NA OMAN WAANDIKIA BARUA YA KISERIKALI KWA RAIS MHE. SAMIA SULUHU HASSAN

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
 
WAZIRI MKUU WA INDIA NA JAPAN PAMOJA NA NAIBU WAZIRI MKUU WA OMAN WAANDIKIA BARUA YA KISERIKALI KWA RAIS MHE. SAMIA SULUHU HASSAN KWA SALAMU ZA RAMBIRAMBI NA PONGEZI 

Mwanza, 24 Machi 2021

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya India Mhe Narendra Modi amemwandikia barua ya kiserikali Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kumpa pole kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.


Katika barua hiyo Mhe. Modi amesema amesikitishwa na kifo cha Dkt. Magufuli kutokana na kumbukumbu zake alipoitembelea Tanzania 2016 na kupata mapokezi yenye ukarimu mkubwa ambapo walizungumza masuala mbalimbali ya kimaendeleo yanayohusu Taifa la India na Tanzania na hata hivi karibuni walipozungumza kwa njia yasimu.


“Nimempoteza rafiki wa karibu na mwenye thamani kubwa na nitamkumbuka kwa namna alivyojitolea kulijenga Taifa lake kwa manufaa ya Watanzania” amesema Mhe. Modi.

Mhe. Modi amemtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan kuwa na moyo wa subra hususani wakati huu anapopokea madaraka ya Urais katika kipindi kigumu cha maombolezo ya Taifa na kumhakikishia kuwa India itaendelea kuwa rafiki mwema kwa Tanzania na Serikali iko tayari kushirikiana naye. 


Mwisho Mhe. Modi amemalizia kwa kusema kwa niaba ya serikali na watu wa India anatoa salamu za rambirambi kwa Mhe. Rais, Familia, Serikali na Watu wote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika tukio jingine Naibu Waziri Mkuu anayeshughulikia Masuala ya Ulinzi wa Serikali ya Oman, Mtukufu Sayyid Shihab bin Tarik bin Taimur Al-Said, akiambatana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Mhe. Sayyid Badr bin Hamad Al Busaidi pamoja na Viongozi wengine wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Oman amesaini kitabu cha maombolezo katika Ubalozi wa Tanzania nchini Oman. 

Katika Salamu zake Mtukufu Sayyid Shihab bin Tarik bin Taimur Al-Said amemuelezea Hayati Dkt. Magufuli kama Kiongozi mchapakazi, mzalendo na mwana maendeleo ambaye Tanzania, Afrika na Dunia itaendelea kumkumbuka. 

Pia amemtakia utendaji kazi mwema na uliotukuka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Viongozi wengine walioandikia barua ya kiserikali kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ni Waziri Mkuu wa Japan Mhe SUGA Yoshihide. Katika barua yake Mhe Yoshihide ameeleza kusikitishwa kwake kufuatia kifo cha Dkt. Magufuli na kwa niaba ya Serikali na watu wa Japan anatoa pole kwa familia, Serikali na Watu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  

Katika barua hiyo amesema Hayati Magufuli enzi za uhai wake amekuwa kiongozi aliyetoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi yake kwa kuhamasisha ujenzi wa viwanda,kutengeneza ajira,na kuweka kipaumbele katika suala la kukuza uchumi usiotegemezi.
 
 “Katika kipindi hiki cha maumivu na huzuni ambacho Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakipitia hivi sasa, Japan iko pamoja na watu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” amesema Mhe. Yoshihide.

 
Mhe. Yoshihide amemalizia barua yake kwa kusema Japan itaendelea kushirikiana na kukuza ushirikiano baina yake na Tanzania

 

Imetolewa na:

Emmanuel Buhohela

Mkurugenzi, Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali.

Downloads File: