Skip to main content
News and Events

WATANZANIA WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA ZA NCHI WANAZOISHI

Watanzania wametakiwa kuwa mabalozi wazuri katika nchi za ugenini kwa kuzingatia na kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi hizo ili kulinda taswira nzuri ya nchi yao. Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu kifo cha Mtanzania, Bw. Nemes Tarimo aliyefariki dunia nchini Urusi. Dkt. Tax amesema Bw. Tarimo alikwenda nchini humo mwaka 2020 kwa ajili ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Moscow Technological University (MIREA) kwa masomo ya Shahada ya Uzamili katika fani ya Business Informatics. 

Akiwa masomoni mwezi Machi 2022 Bw. Tarimo alitiwa hatiani kwa kuhusika na vitendo vya uhalifu na kuhukumiwa kifungo cha miaka saba (7) jela. Dkt. Tax amesema akiwa gerezani, Bw. Tarimo alijiunga na kikundi cha kijeshi cha Urusi cha Wagner kwa ahadi ya kulipwa fedha na kuachiwa huru baada ya vita kumalizika na alifikwa na umauti akiwa katika uwanja wa vita tarehe 24 Oktoba, 2022.

 "Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, si ruhusa kwa raia wake kujiunga na Jeshi la nchi yoyote duniani zaidi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)," alisema Dkt. Tax. Dkt. Tax amesema kuwa mwili wa marehemu umeondoka nchini Urusi tarehe 24 Januari 2023 na unatarajiwa kuwasili nchini muda wowote kuanzia sasa na kuongeza kuwa Serikali imekuwa ikiwasiliana na Serikali ya Urusi ili kuhakikisha mwili wa Marehemu Tarimo unarejeshwa nchini na kukabidhiwa kwa familia yake kwa ajili ya taratibu za mazishi.  

Mhe. Waziri ametoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na Watanzania kwa ujumla kufuatia msiba huo na ameiombea roho ya marehemu Tarimo ilazwe mahali pema peponi. 

Mhe. Waziri ameahidi kwa umma na Diaspora wa Tanzania wakiwemo wanafunzi walioko masomoni nchini Urusi kuwa Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano na kuhakikisha kuwa usalama wao unazingatiwa.

  • Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam kuelezea taarifa ya kifo cha Bw. Nemes Tarimo, mtanzania aliyefariki dunia nchini Urusi
  • Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam kuelezea taarifa ya kifo cha Bw. Nemes Tarimo, mtanzania aliyefariki dunia nchini Urusi
  • Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam kuelezea taarifa ya kifo cha Bw. Nemes Tarimo, mtanzania aliyefariki dunia nchini Urusi