Skip to main content
News and Events
Press Release

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Dodoma, 16 Desemba 2021

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb.) amewasili nchini Uturuki leo tarehe 16 Desemba 2021 kwa ajili ya kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Tatu wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi za Afrika na Serikali ya Uturuki utakaofanyika jijini Instanbul nchini humo kuanzia tarehe 16 hadi 18 Desemba 2021.

Mkutano huu ambao unafanyika kwa mara ya tatu tangu kuanzishwa kwa ushirikiano kati ya Nchi za Afrika na Uturuki mwaka 2008, unalenga pamoja na mambo mengine kufuatilia utekelezaji wa makubaliano na maamuzi mbalimbali yaliyopitishwa na Wakuu wa Nchi kwenye mikutano iliyopita; kuweka mikakati mipya ya ushirikiano kwa kipindi cha mwaka 2021-2026 pamoja na kujadili namna bora ya kuimarisha ushirikiano kati ya nchi za Afrika na Uturuki hususan katika kukuza biashara na uwekezaji. Aidha, maeneo mengine yatakayojadiliwa wakati wa mkutano huo ni pamoja na ushirikiano kwenye sekta ya afya pamoja na ulinzi na usalama.

Mhe. Balozi Mulamula ambaye pia anaongoza ujumbe wa Tanzania, anatarajiwa kuhutubia Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi za Afrika na Uturuki tarehe 18 Desemba 2021 ambapo atawasilisha agenda za Tanzania zenye manufaa kwa nchi kupitia ushirikiano huo. Agenda hizo ni pamoja na fursa za elimu kwa watanzania, kilimo, ujenzi na uchukuzi. 

Ujumbe wa Tanzania unamjumuisha Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Mb.), Mhe. Godwin Mollel, Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe. Lt. Gen. Yacoub Hassan Mohamed, Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu kwenye Umoja wa Afrika na UNECA. Mhe. Innocent Shiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz na Maafisa Waandamizi kutoka Serikalini.

Mkutano huo ambao huandaliwa  kwa ushirikiano kati ya Umoja wa Afrika (AU) na Serikali ya Uturuki, nyaraka kadhaa za utekelezaji zitawasilishwa kwa ajili ya kuridhiwa ikiwemo: Ripoti ya Pamoja ya Utekeelzaji wa Ushirikiano wa Afrika na Uturuki ya mwaka 2015-2020 (The Africa-Turkey Partnership Joint Implementation Report of 2015-2020); Mpango Kazi wa Pamoja wa Afrika na Uturuki wa mwaka 2022-2026 (The Africa-Turkey Joint Action Plan of 2022-2026) na Azimio la Ankara la mwaka 2021 (The Ankara Declaration of 2021).

Kadhalika inatarajiwa kuwa, Mikataba ya Ushirikiano kwenye Sekta ya Elimu kati ya Nchi za Afrika na Serikali ya Uturuki itasainiwa tarehe 17 Desemba 2021.

Mkutano huo wa Tatu  ambao umebeba kauli isemayo: “Ushirikiano Imara kwa Maendeleo na Mafanikio ya Pamoja” utafanyika kwa ngazi tatu, ukianza na Maafisa Waandamizi utakaofanyika tarehe 16 Desemba 2021 na kufuatiwa na mkutanoo wa Mawaziri wa Mambo ya Nje, tarehe 17 Desemba 2021 na kukamilishwa na mkutao wa Wakuu wa Nchi na Serikali hapo tarehe 18 Desemba 2021.

Ushirikiano kati ya Nchi za Afrika na Serikali ya Uturuki ulianzishwa kwa makubaliano ya pande hizi mbili mwezi Aprili 2008 kwa lengo la kuimarisha na kuendeleza maeneo mahsusi ya ushirikiano ambayo yana maslahi mapana kwa ustawi wa nchi za Afrika na Uturuki.

Mkutano wa pili wa Wakuu wa Nchi na Serikali wan chi za Afrika na Uturuki ulifanyika jijini Malabo, Guinea ya Ikweta mwezi Novemba 2014. Mkutano huo uliridhia Azimio la Malabo na Mpango wa Pamoja wa Utekelezaji pamoja na kuandaa Bangokitita inayoainisha miradi ya kipaumbele katika utekelezaji ikiwemo miradi katika sekta ya biashara na uwekezaji, amani na usalama, utamaduni, utalii, elimu, kilimo, miundombinu, nishati, TEHAMA, afya, uchukuzi, ubadilishanaji wa teknolojia pamoj na kuwajengea uwezo vijana.

Mkutano wa Mawaziri kwa ajili ya kutathmini utekelezaji wa Azimio la Malabo na Mpango Kazi wake ulifanyika jijini Istanbul mwezi Novemba 2018 ambapo pamoja na mambo mengine Mawaziri walipitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ushirikiano kati ya Afrika na Uturuki kwa kuzingatia Agenda 2063 ya Umoja wa Afrika pamoja na kuandaa Mkutano wa Tatu wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi za Afrika na Uturuki unaofanyika kuanzia tarehe 16 hadi 18 Desemba 2021.

Mbali na kushiriki mkutano huo, akiwa nchini Uturuki, Mhe. Balozi Mulamula pamoja na mambo mengine anatarajiwa kufanya mikutano na wafanyabiashara pamoja na Watanzania wanaoishi nchini humo (Diaspora). Pia atakutana kwa nyakati tofauti na Taasisi za Uturuki zinazosimamia viwanda vidogo vidogo na masuala ya utalii.

Emmanuel Buhohela

Mkurugenzi, Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali

Downloads File: