Skip to main content
News and Events

MAKAMU WA RAIS WA MAREKANI AMALIZA ZIARA YA KIHISTORIA NCHINI

Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris ameondoka nchini baada ya kumaliza ziara yake ya kihistoria ya siku tatu iliyofanyika kuanzia tarehe 29 hadi 31 Machi 2023 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Akiwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Mhe. Kamala ameagwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango ambaye aliongozana na Mhe. Mama Mbonimpa Mpango na Viongozi wengine wa Serikali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax.

Mhe. Kamala ambaye kwenye ziara hii alifuatana na mwenza wake, Mhe.Douglas Emhoff pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Marekani, pamoja na mambo mengine alikutana na mwenyeji wake Mhe. Rais Dkt Samia tarehe 30 Machi 2023 kwa mazungumzo rasmi ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani na kwa pamoja walizungumza na waandishi wa habari kuhusu makubaliano waliyofikia kwenye mazungumzo yao.

Kupitia ziara hii, Serikali ya Marekani na Tanzania zimeahidi kuimarisha ushirikiano kwenye sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu, usalama wa mitandao, TEHAMA, Afya, usalama wa chakula, usafirishaji huku pia Marekani ikitangaza kutoa Dola za Marekani milioni 500 kupitia Benki ya Exim ili kuwezesha upatikanaji wa kugharamia upelekeaji wa huduma na bidhaa katika sekta za miundombinu, usalama wa mitandao, usafirishaji, teknolojia ya kidigiti, nishati na miradi ya nishati jadidifu.

Kadhalika Serikali ya Marekani ina mpango wa kujenga kiwanda kikubwa cha kuchakata madini ya nikeli yanayotumika kutengeneza betri za umeme wa magari ifikapo mwaka 2026.

Ziara ya Mhe. Kamala nchini ni matokeo  ya juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kukuza na kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani, ililenga pamoja na mambo mengine, kuimarisha ushirikiano hususan kwenye maeneo ya kimkakati ya ushirikiano kama vile biashara, uwekezaji, utalii, elimu, afya na utunzaji wa mazingira, TEHAMA, usafirishaji, bandari na masuala ya utawala bora na demorasia.

  • Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango akisalimiana na Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, muda mfupi kabla ya kondoka nchini baada ya kumaliza ziara yake ya kihistoria ya siku tatu iliyofanyika kuanzia tarehe 29 hadi 31 Machi 2023
  • Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax alipokuwa akiondoka nchini baada ya kuhitimisha ziara yake ya siku tatu nchini.
  • Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris akisalimiana na Mkuu wa Itifaki (Chief of Protocol - CP) katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Yusuph Mndolwa kwenye hafla ya kumuaga Makamu huyo iliyofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam
  • Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris akisalimiana na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mindi Kasiga kwenye hafla ya kumuaga Makamu huyo iliyofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam
  • Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris akisalimiana na Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe. Elsie Kanza kwenye hafla ya kumuaga Makamu huyo iliyofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam
  • Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango akiwa na Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris wakati akimuaga katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam baada ya kumaliza ziara yake ya kihistoria ya siku tatu nchini
  • Viongozi na Watendaji mbalimbali wa Serikali wakimuaga Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris alipokuwa akiondoka nchini baada ya kuhitimisha ziara yake
  • Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax kwenye hafla ya kumuaga Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam
  • Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango akiwa na Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris wakati akimuaga katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam baada ya kumaliza ziara yake ya kihistoria ya siku tatu nchini