Skip to main content
News and Events

BALOZI MULAMULA : WEKENI UTARATIBU WA KUSHUGHULIKIA DIASPORA

BALOZI MULAMULA : WEKENI UTARATIBU WA KUSHUGHULIKIA DIASPORA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) amewataka Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania Nje ya Nchi kuweka utaratibu wa kushughulikia masuala ya Diaspora katika meneo yao ya uwakilishi.

Balozi Mulamula ametoa agizo hilo Jijini Dar es Salaam alipozungumza na mabalozi hao kwa njia ya mtandao kwa lengo la kuwakumbusha na kuwapa tarifa juu ya utendaji kazi wa Wizara na mambo mengine yanayojiri nchini.

 ‘‘Anzisheni utaratibu wa kushughulikia masuala ya Diapora katika maeneo yenu ya uwakilishi, ikiwemo kuratibu mikutano ya mara kwa mara hata kama ni kwa njia ya mtandao’’ amesema Balozi Mulamula.

Waziri Mulamula pia amewataka mabalozi  kuratibu mikutano ya mara kwa mara na diaspora hata kama ni kwa njia ya mtandao ikiwa ni harakati za kuwaweka pamoja na kuwajumuisha katika mipango na harakati za kuiletea nchi maendeleo kupitia Watanzania hao wanaoishi nje ya nchi.

Amewaelekeza mabalozi pia kuhakikisha kuwa wanawatambua Diaspora wa Tanzania duniani kote na kuwawekea mazingira mazuri ya kuwawezesha kuchangia katika maendeleo na uchumi wa taifa.

Waziri Mulamula ameongeza kuwa, Wizara inatambua umuhimu wa Diaspora na kuthamini mchango wao katika maendeleo ya Taifa ndiyo maana  imeamua kuingiza masuala ya Diapora katika  Sera mpya ya Mambo ya Nje.

“Wizara tumehakikisha kuwa masuala ya Diapora yanakuwa sehemu ya Sera ya Mambo ya Nje hii ni kutokana na mchango wa Diapora kwa maendeleo ya Taifa,” amesema Waziri Mulamula.

Balozi mulamula ameongeza kuwa Serikali inalifanyia kazi ombi la Diaspora la kupatiwa hadhi maalum na kuutaka uongozi wa Wizara kuongeza jitihada za kuleta mfumo wa kielektroniki wa kuwasajili Diaspora wote duniani ili kuweza kupata tarifa muhimu na takwimu sahihi.

Katika kikao hicho Waziri Mulamula aliwaelezea mabalozi hao juu ya maandalizi ya Serikali katika kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, utengenezaji wa Sera mpya ya Mambo ya Nje, uanzishwaji wa Idara mpya ya Diplomacia ya uchumi ambayo itakuwa kiungo katika ya wizara, Balozi za Tanzania Nje na Idara na Balozi zetu taasisi nyingine za Umma na Sekta binafsi ili kufanikisha azma ya Serikali katika kutekeleza Diplomasia ya Uchumi na hivyo kujiletea maendeleo.

Aidha, amesema kuwa Serikali imekamilisha ufunguzi wa Konseli Kuu katika Mji wa Lubumbashi - Jamhuri ya Kimemokrasia ya Congo (DRC) na Guangzhou - Jamhuri ya Watu wa China pamoja na kuonesha nia ya kufungua Konseli Kuu katika Mji wa Shanghai na katika Jamhuri ya watu wa China. 

  • Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) akizungumza wakati wa kikao na Mabalozi wa Tanzania nje ya nchi kilichofanyika jijini Dar es Salaam kwa njia ya mtandao.
  • Kiongozi wa mabalozi wa Tanzania nje ya nchi ambaye pia ni Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi Mhe. Irene Kasianju (katikati) akizungumza katika kikao cha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Mabalozi wa Tanzania nje ya nchi kilichofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam kwa njia ya mtandao, kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma Rajab na kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Afrika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Naimi Aziz.
  • Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Diaspora Bi Tagie Mwakawago (kushoto) akizungumza juu ya mfumo wa kielektroniki wa kuwasajili Diaspora katika kikao cha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Mabalozi wa Tanzania nje ya nchi kilichofanyika jijini Dar es Salaam kwa njia ya mtandao.
  • Baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Wizara walioshiriki katika kikao cha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Mabalozi wa Tanzania nje ya nchi kilichofanyika jijini Dar es Salaam kwa njia ya mtandao wakifuatilia kikao hicho.