Skip to main content
News and Events

WAZIRI MULAMULA AZIHAKIKIKISHA USHIRIKIANO TAASISI ZA KIMATAIFA ZENYE MAKAZI YAKE NCHINI

WAZIRI MULAMULA AZIHAKIKIKISHA USHIRIKIANO TAASISI ZA KIMATAIFA ZENYE MAKAZI YAKE NCHINI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb.) amezihakikishia ushirikiano taasisi za kimataifa zenye makazi yake hapa nchini pamoja na kuzitaka kutekeleza kwa tija malengo mahsusi ya taasisi hizo kuwepo nchini Tanzania.

Hayo yamesemwa na Waziri Mulamula alipokutana na Msajili wa Mahakama ya Kimataifa ya Kesi Masalia za iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) na Mauaji ya Halaiki ya iliyokuwa Yugoslavia ya Zamani (ICTY) – (IRMCT) Bw. Abubaccar Tambadou alipomtembelea ofisini kwake jijini Dodoma tarehe 19 Novemba 2021.

‘’Tanzania ikiwa nchi mwenyeji wa mahakama unayoiongoza tutaendelea kutoka ushirikiano ili kuwawezesha kusimamia majukumu yenu kwa ufanisi na kuhakikisha lengo lilokusudiwa la mahakama hii kumaliza kesi zilizobaki pamoja na kuwa kituo cha kumbukumbu kwa kesi hizo linatimia‘’ alisema Mhe. Mulamula.

Waziri Mulamula aliongeza kwa kusema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuthamini heshima ya kuwa mwenyeji wa Taasisi hiyo na kwamba inaendelea kusimamia uhuru na haki za mahakama nchini kama ilivyosaini katika makubaliano mbalimbali ya kimataifa na anakaribisha mashirika mengine ya Kimataifa kuja kujenga nchini kwa kuwa ni mahali salama kuishi na kiutendaji. 

Pia ametumia fursa ya mazungumzo hayo kuwakaribisha watanzania na wageni wanaofanya tafiti kuhusiana na taasisi hiyo na nyingine za kimataifa zinazohusiana kwa namna moja au nyingine kiutendaji na mahakama ya IRMCT kuja kwa ajili ya kufanikisha tafiti zao.

Bw. Abubacaar amefanya ziara hiyo kwa ajili ya kujitambulisha kufuatia kuteuliwa kwake hivi karibuni kuwa Msajili wa Mahakama hiyo, ambapo pamoja na mambo mengine alipata nafasi ya kueleza majukumu ya Mahakama sambambamba na maboresho ya kiutendaji yanayotarajiwa kufanywa na mahakama hiyo.

“Mahakama inashukuru kwa ushirikiano unaoendelea kutolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na itaendelea kutoa taarifa za mara kwa mara pale inapobidi ili kuiwezesha nchi mwenyeji kuwa na uelewa wa pamoja na mahakama kiutendaji” alieleza Bw. Abubaccar

Wataalamu wengine walioshiriki katika mazungumzo hayo ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab, Mkurugenzi Kitengo cha Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Caroline Chipeta, Mkuu wa Utawala wa Mahakama ya IRMCT, Bw.  David Falces, na Mwanasheria kutoka IRMCT, Bi. Tully Mwaipopo.

Mwaka 2010 Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, lilipitisha Azimio nambari 1966 la kuanzisha Mfumo wa Kimataifa utakaomalizia mashauri ya Masalia kwa iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya Rwanda (ICTR) yaliyotokea mwaka 1994 na Mauaji ya Halaiki yaliyotokea katika iliyokuwa Yugoslavia ya Zamani (ICTY).  Katika azimio hilo Baraza kuu lilibainisha wazi kwamba Arusha itakuwa Makao Makuu ya tawi hilo jipya la IRMCT na The Hague kuwa makao makuu ya Tawi Jingine.

  • Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) na Msajili wa Mahakama ya Kimataifa ya Kesi Masalia za Mauaji ya Kimbari Bw. Abubacarr Tambadou wakiwa katika picha ya pamoja.
  • Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akifafanua jambo alipokuwa katika mazungumzo na Msajili wa Mahakama ya Kimataifa ya Kesi Masalia za Mauaji ya Kimbari (IRMCT) Bw. Abubacarr Tambadou jijini Dodoma.
  • Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akimsikiliza Msajili wa Mahakama ya Kimataifa ya Kesi Masalia za Mauaji ya Kimbari Bw. Abubacarr Tambadou walipokutana kwa mazungumzo jijini Dodoma.