Skip to main content
News and Events

TANZANIA YASISITIZA KUUNGA MKONO, KUENDELEZA UHUSIANO NA CHINA

Tanzania imesisitiza kuunga mkono, kuendeleza ushirikiano, uhusiano na mshikamano ambao China imekuwa ikiuonesha kwa nchi za Afrika.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula alipozungumza katika Mkutano wa nane wa Mawaziri wa ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika Jijini Dakar Senegal Novemba 29-30, 2021.

Amesema kwa kuangalia yaliyotokea katika kipindi hiki kigumu ambacho dunia inakipitia, China imekuwa ikishirikiana na Afrika kwa kutoa misaada mikubwa  ya fedha, wataalamu na vifaa kwa nchi za Afrika katika nyanja mbalimbali na kuwa na ushirikiano ambao umenufaisha pande zote.

Amesema kwa upande wa Tanzania China imekuwa ikisaidia katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati  ambayo imekuwa ikifanyika kwa kushirikiana na makampuni yao makubwa yanayowekeza chini .

Aidha Tanzania imeiomba China kuweka msisitizo mkubwa  katika sekta ya afya hasa katika kupambana na janga la ugonjwa wa korona unaosababishwa na virusi vya COVID 19 kwa kujengewa viwanda na kupatiwa uwezo wa kuzalisha chanjo hizo na dawa nyingine wenyewe.  

Waziri Mulamula amepongeza kauli ya Rais wa China Mhe. Xi Jinping ya kuwa nchi hiyo itatoa dozi billioni moja zaidi kwa nchi za Afrika ili kuziwezesha nchi  za Afrika kufikia lengo la kutoa chanjo kwa angalau asilimia 60 kwa watu wake ifikapo mwaka  2022.

“Tanzania imepokea taarifa hizo kwa mikono miwili na tunaishukuru serikali ya China kwani iliipatia Tanzania chanjo laki tano na tunategemea kupata  chanjo nyingine, na sasa kwa tangazo hilo China wametuhakikishia kwamba tutapata chanjo kwa kiasi kile tunachohitaji”, amesema Balozi Mulamula.

Mkutano huo ulijumuisha viongozi na wawakilishi kutoka Bara la Afrika na China na kuangalia ambavyo China ilivyotekeleza hatua za ushirikiano kwa kipindi cha miaka mitatu cha 2018-2021 kwenye  maeneo ya ujenzi wa maeneo maalum ya viwanda barani Afrika, ujenzi wa miundombinu ya nishati, usafirishaji, habari na mawasiliano, kukuza wigo  wa biashara kati ya China na mataifa ya Afrika.

Maeneo mengine ni kampeni ya mapinduzi ya kijani, mpango maalum wa mafunzo ya ufundi, kuboreha sekta ya Afya, ulinzi na usalama na ushirikiano katika masuala ya habari, utamaduni sanaa na michezo.

  • Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akifuatilia Mkutano wa nane wa Mawaziri wa ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika Jijini Dakar Senegal Novemba 29-30 2021.
  • Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akimsikiliza mshiriki wakati wa Mkutano wa nane wa Mawaziri wa ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika Jijini Dakar Senegal Novemba 29-30 2021.
  • Washiriki wa Mkutano wa nane wa Mawaziri wa ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika Jijini Dakar Senegal Novemba 29-30 2021 wakifuatilia mkutano huo.