Skip to main content
News and Events
Press Release

TAMKO LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KUPINGA VIKWAZO DHIDI YA JAMHURI YA ZIMBABWE

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 

TAMKO LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KUPINGA VIKWAZO DHIDI YA JAMHURI YA ZIMBABWE

Dodoma, 25 Oktoba 2021

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaunga mkono tamko la Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika (SADC) la kupinga vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Zimbabwe ilivyowekewa na mataifa ya Ulaya na Marekani. 

Vikwazo hivyo vimerudisha nyuma uwezo wa Jamhuri ya Zimbabwe kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na vina athari kubwa zaidi kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa watu wa Zimbabwe hususan makundi maalum ya wanawake, watoto na wazee.

Vikwazo hivyo licha ya kuiathiri Zimbabwe, vina athari pia kwa Jumuiya za Kikanda na Kimataifa kwa kuwa vinainyima fursa nchi hiyo kushirikiana na Nchi Wanachama wa SADC na Umoja wa Afrika (AU) kibiashara na katika utekelezaji wa miradi ya ushirikiano ya Maendeleo.

Aidha, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaunga mkono hatua ya Umoja wa Mataifa (UN) kumwagiza Mjumbe wake, Profesa Alena Douhan kwenda nchini Zimbabwe kwa ajili ya kukutana na Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mhe. Emmerson Mnangagwa, Viongozi wa Taasisi za umma na Mashirika ya kiraia kwa lengo la kutathmini athari za vikwazo hivyo. Hii ni hatua chanya ya uwepo wa uwezekano wa Jamhuri ya Zimbabwe na Mataifa ya Ulaya na Marekani kukutana katika meza ya mazungumzo ili kuona namna ya kuondoa vikwazo hivyo.  

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawapongeza viongozi na Wanachama wa SADC kwa kuendelea kuyatumia majukwaa ya kitaifa, kikanda na kimataifa kupaza sauti dhidi ya vikwazo hivi kwa maslahi mapana ya Kanda. 

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuitetea Jamhuri ya Zimbabwe ikiwa ni sehemu ya historia yetu ya kupigania ukombozi wa Bara la Afrika.

Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika tarehe 17 – 18 Agosti 2019 Dar es Salaam, Tanzania uliidhinisha tarehe 25 Oktoba ya kila mwaka kuwa siku kwa nchi Wanachama wa SADC kupaza sauti kupitia majukwaa ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa kupinga vikwazo ambavyo mataifa ya Ulaya na Marekani yameendelea kuiwekea Jamhuri ya Zimbabwe kwa takribani miaka 18.

 

Emmanuel Buhohela,

Mkurugenzi, Kitengo cha Mawasiliano

 

Downloads File: