Skip to main content
Kuhusu Wizara

About the Ministry

Historia ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilianza tangu mwaka 1961 mara tu Tanzania (Tanganyika wakati huo)  ilipopata uhuru. Mpaka Desemba 1963, ilikuwa Idara chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Mwaka 1964 ikawa wizara kamili kwa jina la Wizara ya Mambo ya Nje.

Kwa miongo minne tangu katika miaka ya sitini, shughuli za Wizara zimekuwa zikiendeshwa kwa kutumia waraka namba 2 wa mwaka 1964. Waraka huu katika eneo la Sera ya Mambo ya Nje ulitoa kipaumbele katika maeneo ya usawa, kujitegemea, amani duniani na kwa kuangalia misingi ya uchumi wa kijamii. 

Kwa mfano changamoto za utawala wa kikoloni na ukoloni mambo leo, uhasama wa nchi zenye nguvu duniani, mazingira hafifu ya uchumi kwa nchi zinazoendelea na udhaifu wa nchi za kiafrika katika kujitegemea zilihitaji hatua hiyo. Sera hii ilitimiza malengo  ya nchi kwa miaka kadhaa.

Hata hivyo, mabadiliko ya mwelekeo wa kisiasa na ya ki-uchumi duniani katika miaka ya themanini na tisini yalipelekea marudio ya Sera ya Mambo ya Nje na hatimaye ufafanuzi mpya wa majukumu ya Wizara. Mabadiliko mapya yalijumuisha hitimisho la vita baridi baina ya nchi zenye nguvu duniani na mahusiano mapya kufuatia matokeo yalioyofuata. Kwa mfano mwelekeo mpya wa masoko kimataifa, mwelekeo mpya wa katika utoaji wa misaada, uwekezaji, ukumbatiaji wa demokrasia ya vyama vingi, haki za binadamu, utawala bora, kuibuka kwa ushirikiano katika vita ya ugaidi, uhamiaji haramu, uhifadhi wa mazingira pamoja na ukuaji wa sayansi na teknolojiia,  vilipelekea hatua mbalimbali kama vile mahusiano ya kikanda na kimataifa kuangaliwa upya kupitia Sera ya Mambo ya Nje.

Dira: Kuwa mwenezaji mzuri wa uchumi wa Tanzania na maslahi mengine ya taifa nje ya nchi

Dhamira: Kusimamia na kutekeleza diplomasia thabiti ambayo itachangia katika shughuli za kiuchumi na kuwezesha mageuzi ya haraka na maendeleo endelevu ya Tanzania.