Skip to main content
Press Release

Taarifa kuhusu ziara ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola nchini


Taarifa kuhusu ziara ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola nchini
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Mheshimiwa Patricia Scotland anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 10 hadi 12 Agosti, 2017. 

Lengo la ziara hiyo ni kueleza Viongozi wa Ngazi za Juu wa Taifa kuhusu  mageuzi yanayofanywa na Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola na vipaumbele vya Jumuiya hiyo kwa sasa; Hatua zinazochukuliwa ili kuimarisha kazi za Jumuiya hiyo na kutoa taarifa kuhusu Mkutano wa Wakuu Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola unaotarajiwa kufanyika London, Uingereza mwezi Aprili, 2018.

Mageuzi hayo yanajumuisha kuondoa vyeo vya Naibu Makatibu Wakuu watatu na kupunguza idadi ya Wakurugenzi kutoka 12 hadi 6. Mageuzi haya yataiwezesha Jumuiya kuokoa kiasi cha Pauni milioni 3 kwa mwaka. Mageuzi mengine ni ya kuanzisha nafasi tano za Maafisa Waandamizi kutoka maeneo ya kijiografia ya Jumuiya ya Madola kwa maana ya Afrika, Ulaya na Amerika, Karibeani, Asia na Pacific Kusini. Nafasi hizi zitaziba zile za Naibu Makatibu Wakuu.

Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Scotland atakutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa mazungumzo tarehe 11 Agosti, 2017, Ikulu, Dar es Salaam.

Aidha, Mhe. Scotland ataonana na Mawaziri mbalimbali kwa nyakati tofauti ikiwa ni pamoja na Mhe. Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. January Makamba, Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.

Mhe. Scotland na ujumbe wake wataondoka nchini tarehe 12 Agosti, 2017 kuelekea Msumbiji.

Historia fupi kuhusu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Mhe. Patricia Scotland alichaguliwa kwenye nafasi hiyo mwezi Novemba, 2015 wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali (CHOGM) uliofanyika nchini Malta. Kabla ya kuchaguliwa kwake Jumuiya hiyo iliongozwa na Bw. Kamalesh Sharma ambaye alishikilia nafasi hiyo kuanzia mwaka 2008 hadi 2016.

Jumuiya ya Madola

Jumuiya ya Madola ni Umoja ulioanzishwa mwanzoni mwa karne ya 20. Jumuiya hiyo inajumuisha Uingereza pamoja na nchi ambazo zilikuwa koloni la Uingereza. Uanachama wa Jumuiya hiyo kwa sasa hauzingatii kigezo cha koloni hivyo nchi yoyyote inaweza kujiunga na Jumuiya ya Madola kama itapenda. Malkia ndiye Kiongozi Mkuu wa Jumuiya ya Madola.

Jukumu kubwa la Jumuiya ya Madola ni kuhakikisha nchi wanachama zinajikwamua kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa kutumia jukwaa la majadiliano, makubaliano na utekelezaji.

Ushiriki wa Tanzania katika Jumuiya ya Madola


Jumuiya ya Madola inajumuisha nchi 52 Tanzania ikiwa ni mwanachama wa Jumuiya hiyo tangu mwaka 1961. Tangu kujiunga kwake, Tanzania imewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Jumuiya hiyo. Miongoni mwa nafasi hizo ni ile ya Uenyekiti wa Kundi la Mawaziri la Utekelezaji la Jumuiya ya Madola (Commonwealth Ministrial Action Group (CMAG). Kundi hili lilijumuisha Mawaziri tisa ambao walipewa jukumu la kusimamia misingi mikuu ya Jumuiya ya Madola. Tanzania ilishikilia nafasi hii kuanzia mwaka 2013 hadi 2015.

Pia Tanzania ni mjumbe kwenye Bunge la Jumuiya ya Madola (CPA). Kutokana na mchango mkubwa wa Tanzania kwenye Jumuiya ya Madola, kuanzia mwaka 2007 hadi 2014 Marehemu Dkt. William F. Shija aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Bunge hilo. Aidha, mwaka 2009 Tanzania ilikuwa mwenyeji wa Mkutano wa 55 wa Bunge la Jumuiya ya Madola uliofanyika Jijini Arusha.

Aidha, miongoni mwa faida ambazo Tanzania imepata kutokana na kujiunga na Jumuiya hii ni pamoja na kukuza biashara na uwekezaji na nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola zikiwemo Uingereza, India, Kenya na Afrika Kusini. Nchi hizi ni miongoni mwa  nchi  zilizowekeza zaidi kwa biashara nchini Tanzania.

Tanzania imenufaika kwenye masuala ya  Teknolojia kupitia Taasisi ya Commonwealth of Learning (COL) ambayo inahamasisha mafunzo ya wazi na ya mbali miongoni mwa nchi wanachama. Pia Jumuiya ya Madola ina  mchango mkubwa kwenye mageuzi katika  Sekta ya Umma na utoaji mafunzo, kozi na misaada mbalimbali ya kiufundi kupitia Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola na Mfuko wa ushirikiano wa Kiufundi wa  Jumuiya ya Madola (CFTC).

Tanzania imekuwa mshiriki mzuri wa michezo maarufu ya Jumuiya ya Madola ambayo inalenga kuhamasisha ushirikiano na urafiki miongoni mwa nchi wanachama. Itakumbukwa kuwa mwaka 1974 Bw. Filbert Bayi alivunja rekodi  kwa kukimbia mita 1,500 mashindano yaliyofanyika huko Christchurch, New Zealand. 

Michezo ya Madola hufanyika kila baada ya miaka minne. Tanzania inajiandaa kushiriki kwenye michezo  ya Madola itakayofanyika mwezi Aprili, 2018 huko Gold Coast, Australia.

-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dar es Salaam
09 Agosti, 2017