Skip to main content
News and Events

JAJI IMANI ABOUD WA TANZANIA ASHINDA UCHAGUZI WA MAJAJI WA MAHAKAMA YA AFRIKA YA HAKI ZA BINADAMU

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

JAJI IMANI ABOUD WA TANZANIA ASHINDA UCHAGUZI WA MAJAJI WA MAHAKAMA YA AFRIKA YA HAKI ZA BINADAMU NA WATU

Mkutano wa 33 wa Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Afrika unaoendelea Jijini Nouakchott, Mauritania kwa siku mbili, leo tarehe 29 Juni, 2018 umefanya uchaguzi wa Majaji wanne wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu.

Mgombea wa Tanzania Mhe. Jaji Imani D. Aboud ameshinda uchaguzi huo kwa kura 47 kati ya kura 50 zilizopigwa na kufanikiwa kuchukua nafasi ya Jaji Solomy Balungi Bossa wa Uganda aliyejiuzulu nafasi hiyo kabla ya kumaliza kipindi chake.

Kwa ushindi huo, Mhe. Jaji Aboud atakuwa Jaji wa Mahakama hiyo akiwakilisha Kanda ya Afrika Mashariki kwa kipindi cha miaka miwili.

Majaji wengine walioshinda kwenye uchaguzi huo ni pamoja na Jaji Kioko Ben (Kenya), Jaji Tchikaye Balise (Jamhuri ya Congo), na Jaji Anukam Stella Isibhkhomen (Nigeria).

Ushindi huu unadhihirisha uwezo mkubwa alionao Mhe. Jaji Aboud na heshima kubwa iliyonayo nchi yetu katika Bara la Afrika.

-Mwisho-

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,

Dar es Salaam, 29 Juni, 2018

Downloads File: