Skip to main content
News and Events

Dkt. Mahiga amwakilisha Rais katika Jukwaa la Uchumi Duniani


Tanzania imesisitiza umuhimu wa kukabili uhaba wa chakula kwa kuzalisha mazao kwa kutumia utalaamu wa kisasa kwa kuwapatia wakulima pembejeo na masoko ya uhakika ya chakula cha ziada.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb) wakati wa kuchangia mjadala unaohusu uhakika wa chakula na changamoto za uhaba wa chakula duniani katika mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani (World Economic Forum-WEF) unaofanyika Davos, Uswisi kuanzia tarehe 22 hadi 25 Januari 2019.
Mhe. Mahiga alimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika jukwaa hilo ambalo kaulimbiu ya mwaka huu ni Kutengeneza Mazingira ya Utandawazi wa Dunia kwa ajili ya Mapinduzi ya Kisasa ya Nne ya Viwanda“Shaping a Global Architecture in the Age of the Fourth Industrial Revolution”.
Katika mkutano huo, ajenda kuu zilizojadiliwa ni pamoja na Mapinduzi ya Nne ya Viwanda, Agenda ya Afrika ya Maendeleo, Hali ya Ulinzi na Usalama Pembe ya Afrika, changamoto za biashara ya kimataifa, ushirikiano wa Bara la Ulaya na Afrika katika ajenda mpya ya maendeleo.
Tanzania ilialikwa kuchangia mjadala unaohusu uhakika wa chakula na changamoto za uhaba wa chakula duniani pamoja na ajenda ya uwezeshaji wa mawasiliano ya simu za mkononi. Katika ajenda hiyo, Tanzania ilitoa wito wa umuhimu wa teknolojia katika kuboresha utaalamu katika sekta ya kilimo kwa ajili ya kuwawezesha wakulima wadogo waliopo vijijini.
Hili ni Jukwaa la pekee ambalo linakutanisha kwa pamoja Viongozi wa Serikali kutoka mabara yote duniani, Taasisi na Mashirika ya Kimataifa, Viongozi wa Makampuni Makubwa ya Kibiashara kwa ajili ya kujadili maendeleo na mwelekeo wa uchumi duniani.
Kando ya Mkutano huo, Mhe. Dkt. Mahiga alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa mashirika na makampuni ambayo yapo Tanzania na yanayohitaji kupanua wigo kama vile Tigo na General Electric na makampuni yanayotafuta fursa za kuwekeza Tanzania. Aidha, alikutana na Rais wa WEF, Mhe. Borge Brende ambapo aliahidi kushawishi wawekezaji kuwekeza Tanzania na kuandaa Jukwaa la wawekezaji wa kimataifa la Tanzania ili waweze kuwekeza Tanzania.
Viongozi wengine waliokutana na Waziri Mahiga ni pamoja na; Bw. Scott Strazik, Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Gesi yenye Makao makuu yake Atlanta, Georgia- Marekani; Bw. Richard Hatchett, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kupambana na magonjwa ya Mlipuko (Coalition for Epidermic Preparedness Innovations); Bi. Rachel Samren, Makamu wa Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya Millicom ambayo TIGO ni Tawi la Kampuni hiyo, na Bw. Mohamed Al-Beity, Mtanzania aliyetambuliwa na Jukwaa la Uchumi Duniani kwa mradi wa kutangaza Utalii wa Tanzania kwa njia ya Mtandao (Tanzania Digital Tourism).