|
Wizara yatoa ufafanuzi kuhusu madai ya CHADEMA
Posted: Thursday March 17, 2011 2:41 PM BT
Taarifa kwa vyombo vya Habari
1.0 Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu baadhi ya hoja zinazoandikwa na vyombo vya habari kuhusu Mkutano wa Mhe. Bernard Membe (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na waandishi wa habari tarehe 12 Machi, 2011 Wizarani. 2.0 Katika mkutano ule, Mhe. Waziri Membe aliwaeleza waandishi wa habari mambo manne:- 2.1 Salaam za rambirambi za Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Waziri Mkuu wa Japan, Mhe. Naoto Kan kutokana na vifo na maafa yaliyotokana na tetemeko la ardhi nchini humo, 2.2 Maamuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika kuhusu mgogoro wa Ivory Coast, 2.3 Kutengemaa kwa hali ya kisiasa nchini Misri na 2.4 Kurejeshwa nyumbani kwa Watanzania waliokuwa wanashikiliwa na Maharamia wa kisomali na baadaye kuokolewa nchini Madagascar. 3.0 Masuala hayo ndiyo yalikuwa agenda ya kukutana na Waandishi wa habari. Katika kipindi cha Maswali na majibu, Mhe. Waziri aliulizwa maswali kadhaa, likiwemo swali kwamba kuna ujumbe wa simu za mkononi unaosambazwa kuwa baadhi ya nchi za Jumuiya ya Ulaya zinatuhumiwa kukifadhili Chama kimoja cha siasa nchini kuleta machafuko na kwamba raia wa nchi wanachama wa Jumuiya Ulaya wanakuwa na wasiwasi juu ya usalama wao. Mwandishi huyo alitaka kujua iwapo Serikali ina habari na imechukua hatua juu ya tuhuma hizo. Majibu ya Mhe. Waziri yalikuwa mafupi, "Taarifa hizo tumezipata na tumezipeleka kwenye vyombo vinavyohusika kwa uchunguzi, na tukipata majibu tutaawaarifu". Mhe Waziri hakuitaja nchi wala Chama kinachotuhumiwa. 4.0 Wizara imeshangazwa kuona kwamba baadhi ya Vyombo vya Habari na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) vimeamua kwa makusudi kupotosha ukweli na kujenga hisia kwamba Mhe. Waziri aliitisha mkutano ule kuelezea tuhuma hizo, jambo ambalo si kweli. 5.0 Wizara haikuwa na sababu yoyote ya kulileta suala hilo kwenye Vyombo vya Habari kwa sababu ziko taratibu chini ya Mkataba wa Kimataifa wa Vienna kuhusu Mahusiano ya Kidiplomasia wa 1961, unaoainisha taratibu na hatua za kidiplomasia za kuchukuliwa dhidi ya vitendo vya namna hiyo pindi uchunguzi unapokamilika. 6.0 Wizara inasikitishwa sana na upotoshwaji huu wa waziwazi. Imetolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano na Ushirikiano wa Kimataifa 16 Machi, 2011. |