|
Waziri kukutana na Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai
Posted: Wednesday June 03, 2009 3:24 PM BT
Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb) tarehe 1 Juni, 2009 amekutana na Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai, Mhe. Sang-Hyun Song
Katika mazungumzo hayo, Mhe. Waziri Membe alimkaribisha mgeni wake na kutumia fursa hiyo kumueleza Mhe. Sang-Hyun Song sababu zilizoifanya Tanzania wakati ikiwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika kutoiunga mkono ICC katika uamuzi wake wa kumkamata na kumfikisha mbele ya sheria Rais wa Sudan, Mhe. Omar al Bashir. Kimsingi, Mhe. Waziri Membe alieleza kwamba Tanzania haipingi hatua zozote za kisheria dhidi ya kiongozi yeyote, ila inaona kukamatwa kwa Rais Omar al Bashir wakati huu kunaweza kuathiri mpango wa kutafuta Amani Kusini mwa Sudan na mchakato wa Amani katika jimbo la Darfur. Kwa Upande wake, Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai, alimshukuru Mhe. Waziri Membe kwa ufafanuzi huo hususan taarifa kwamba Tanzania haipingi tuhuma zinazomkabili Rais Omar al Bashir. Aidha, Kiongozi huyo wa ICC alitumia fursa hiyo kuwasilisha rai kutoka Mahakama hiyo kuiomba Tanzania kukamilisha taaratibu za kuridhia Mkataba wa Roma kwa kutengeneza sheria maalum zitakazosimamia utekelezaji wa mkataba huo. ICC imeiomba Tanzania kusaini mkataba wa kupokea wafungwa watakaohukumiwa na mahakama hiyo (Enforcement of Sentencing Agreement). |