|
Taarifa ya Waziri Membe kwa Waandishi wa Habari
Posted: Thursday September 30, 2010 11:39 AM BT
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU ZIARA YA KIKAZI YA MHE BERNARD MEMBE, WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA NEW YORK, 2010.
Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe alifanya ziara ya kikazi nchini Marekani kuanzia tarehe 20 hadi 27 Septemba, 2010 kuhudhuria Kikao cha 65 cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNGA) jijini New York. Ujumbe wa Tanzania katika Kikao hicho uliongozwa na Mhe. Mizengo Peter Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyemwakilisha Mhe Rais Jakaya Mrisho Kikwete. Kikao cha UNGA kilitanguliwa na Mkutano Maalum wa Wakuu wa Nchi kutathmini mafanikio ya utekelezaji wa Mpango wa Malengo ya Milenia (High Level Summit on MDGs) kilichofanyika tarehe 20-22 Septemba. Aidha, kulikuwa na mikutano mingine sambamba (side events) mingi ikigusia masuala mtambuka kama malaria, utokomezaji wa silaha (disarmament) na mingineyo. Masuala muhimu yaliyojitokeza: 1. Mafanikio na Changamoto katika Utekelezaji wa Malengo ya Milenia Lengo kuu la Mkutano huo lilikuwa ni kutathmini utekelezaji na kutafuta namna ya kutoa msukumo mpya katika kukamilisha ngwe ya mwisho ya miaka mitano iliyosalia ya kukamilisha mpango huo wa miaka 15 (2010-2015). Yafuatayo yalijitokeza: Dunia bado iko nyuma katika utekelezaji wa Malengo ya Milenia. Mafanikio yameonekana katika baadhi ya malengo huku kukiwa na kulegalega katika maeneo mengine. Dunia inaweza isifikie malengo hayo ikiwa. Jitihada za ziada na rasilimali zaidi hazitaelekezwa katika utekelezaji wa malengo hayo. Kufuatia changamoto hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliwasilisha Mpango mpya wa utokomezaji wa vifo vya akina mama na watoto, yaani, Secretary-General’s Global Strategy for Women’s and Children’s Health. Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu wa Norway ni wadau waanzilishi wa mpango huo ambao katika uzinduzi wake ahadi za kiasi cha US$ 40 milioni zilitolewa. a. Ifikapo mwaka 2015, mpango huo unatarajia kuzuia vifo vya watoto milioni 16 duniani kote: kuzuia mimba milioni 33 za wasichana wadogo zinazoweza kuzuilika; kuzuia vifo zaidi ya 700,000 vinavyotokana na uzazi; na kukinga watoto mil 120 dhidi ya kifaduro (pneumonia). b. Dunia na hasa nchi za kiafrika zimepiga hatua kubwa kwenye malengo namba 4 na 5 yanayohusu kupunguza vifo vya kina mama na watoto (maternal and child health). Hata hivyo mafanikio hayo hayakuvuka lengo. c. Maeneo mengine hususan elimu, usawa wa kijinsia na utokomezaji wa magonjwa kama Ukimwi, Malaria, TB na Polio nayo yamepata mafanikio makubwa katika baadhi ya nchi. Ripoti zinataja na kutolea mfano mafanikio ya Tanzania katika kupambana na malaria hususan Zanzibar ambako ugonjwa huo umetokomezwa kwa asilimia 99 ( Rais Jakaya Kikwete pia ni Mwenyekiti wa Mpango wa Viongozi wa Afrika dhidi ya Malaria- ALMA). Aidha walipongeza pia mafanikio ya Tanzania katika mpango wake wa kupanua elimu ya msingi na kuongeza idadi ya watoto wanaoingia darasa la kwanza kila mwaka kwa kuzingatia urari wa jinsia (Gender Balance). d. Tanzania ilipatiwa Tuzo maalum ya Umoja wa Mataifa kwa mafanikio makubwa iliyopata katika uandikishaji wa watoto wenye umri wa kwenda shule kwa zaidi ya asilimia 95, kabla ya kufikia mwaka 2015. 2. Mkutano wa Wakuu wa Nchi kuhusu Hali ya Somalia Mkutano wa Wakuu wa Nchi kuhusu Somalia (Mini Summit on Somalia) uliitishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa tarehe 23 Septemba kujadili hali ya Somalia na mustakhabali wa amani wa nchi hiyo. Mkutano huo uliitishwa kujadili hali ya Somalia kuelekea mwishoni mwa kipindi cha Serikali ya Mpito (Transitional Federal Goverment- TFG). Yafuatayo yalijitokeza: a) Mkutano ulionyesha kusikitishwa na kudorora kwa umoja katika Serikali ya Somalia kulikopelekea kufukuzwa kwa Waziri Mkuu wa Serikali hiyo. Mkutano ulimhimiza Rais wa Somalia kuharakisha uteuzi wa Waziri Mkuu mpya na kukamilisha kwa amani mchakato wa kutengeneza Katiba mpya; b) Mkutano ulipongeza juhudi za IGAD katika kutafuta suluhu. Mkutano ulipongeza pia nchi za Burundi na Uganda zilizojitolea majeshi kwenye AMISOM. Mkutano ukihimiza nchi nyingine zilizoahidi kutoa majesho kufanya hivyo mapema iwezekanavyo; c) Mkutano uliitaka UN na hasa Baraza Kuu la Usalama kutojitoa jukumu lake katika kutafuta amani ya kudumu Somalia. Aidha, ulipongeza uteuzi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuanzisha Ofisi Maalum ya kushughulikia na kuratibu shughuli za UN nchini Somalia na kumteua aliyekuwa Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Dkt. Augustine Mahiga kuwa Mkuu wa Ofisi hiyo ya UN yenye makazi yake Nairobi; d) Mkutano ulilaani vitendo vya Al- Shabaab vya kigaidi vilivyofanyika Uganda na kutaka kushirikishwa kwa serikali za Somaliland na Puntland katika kudhibiti hali ya usalama ndani ya Somalia na katika pwani ya Somalia kwa upande wa ugaidi; e) Viongozi wengi haswa kutoka nchi za kiafrika walitaka rasilimali zielekezwe zaidi katika kugharamia nchi zitakazochangia majeshi ya AMISOM ili kudhibiti usalama ndani ya Somalia na si kupeleka rasilimali nyingi kwenye suala la uharamia kwa kuwa suala la uharamia linatokana na kulegalega kwa usalama ndani ya Somalia. 3. Mchakato wa Kura ya Maoni nchini Sudan Kama mnavyofahamu, Sudan inatarajiwa kuendesha kura ya maoni mapema mwakani kuamua hatima ya Sudan Kusini ikiwa ni kilele cha utekelezaji wa mpango wa miaka mitano wa amani kati ya Sudan Kaskazini na Sudan Kusini maarufu kama Comprehensive Peace Agreement (CPA). Katika taarifa yake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amemteua Mhe. Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa mwangalizi wa Umoja wa Mataifa katika kura hiyo ya maoni. Mhe Rais Mkapa ataongoza jopo la wataalamu kutoka UN na kuwasilisha taarifa yake kwa Katibu Mkuu wa UN. Uteuzi huu ni heshima kubwa kwa Mhe. Mkapa na nchi yetu. 4. Suala la Madagascar Suala la Serikali ya Madagascar kutaka kupatiwa nafasi ya kushiriki katika mjadala (General Debate) wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilijitokeza tena katika kikao hichi. Jitihada kama hizo zilizimwa katika kikao kilichopita na nchi wanachama wa Jumuiya ya SADC kutokana na Serikali ya Rais Rajoelina kuwekewa vikwazo na SADC kutokana na hatua yake ya kupokonya madaraka kwa njia haramu, na kukaidi maazimio ya SADC ya kumtaka kuachia madaraka na kuitisha uchaguzi mpya. Baada ya kushindwa kwa jaribio lao la kutaka Rais Rajoelina kushiriki mjadala mwaka jana, katika kikao hiki, Madagascar ikiungwa mkono na baadhi ya nchi za Magharibi ilijaribu turufu yake kwa kuwasilisha ombi kwa Rais wa Baraza hilo wakitaka Waziri wa Mambo ya Nje wa Madagascar apatiwe fursa hiyo. Nchi za SADC pamoja na Mwenyekiti wa AU (Malawi) walikutana New York na kuwasilisha kwa Rais wa UNGA shinikizo na azma yao ya kumzuia mwakilishi wa Madagascar kutoshiriki mjadala kwa kutumia sheria na taratibu za Baraza hilo ( Rules of Procedure). Baada ya kupima upepo wa shinikizo la SADC, Madagascar iliamua kusalimu amri na kuondoa ombi lake kukwepa kujirudia kwa aibu waliyopata kwenye kikao kilichopita baada ya Azimio lililowasilishwa na SADC dhidi ya Madagascar kupitishwa na Baraza hilo kwa kauli moja bila kupingwa. Haya ni mafanikio makubwa kwani yatatuma ujumbe mkali kwa Serikali ya Madagascar na viongozi wengine Afrika wanaotumia njia haramu kuingia madarakani. 5. Mpango Mpya wa Marekani katika kutekeleza MDGs Kukuza Mahusiano kati ya Tanzania na Marekani Serikali ya Marekani imetangaza Mkakati wake mpya katika kukamilisha duru ya mwisho ya utekelezaji wa MDGs (U.S. Global Development Policy). Mkakati huo ulitangazwa na Rais Barack Obama wa Marekani katika Mkutano wa Malengo ya Milenia. Katika hotuba yake, Rais Obama alisisitiza azma ya Serikali yake kutazama upya vigezo vya nchi yake katika kutoa misaada ya kimaendeleo, kiasi inachotoa,aina ya misaada na walengwa wa misaada hiyo. Katika mkakati mpya, Serikali ya Marekani itazingatia mahitaji na vipaumbele vya nchi husika katika utoaji wa misaada yake na si kutazama tu kiasi cha fedha inachotumia/kinachotumia. Aidha, itashirikiana na zile Serikali zinazoendeleza sera za uwazi, uwajibikaji na utawala bora. Katika hili, Rais Obama aliitaja Tanzania kuwa nchi ya kupigiwa mfano katika eneo hili. Tayari Tanzania inafaidika na Mpango wa MCC wa Marekani ikiwa ni moja ya nchi chache za Afrika. Tanzania inayo nafasi kubwa zaidi ya kufaidika na misaada ya kimaendeleo katika Mkakati mpya wa Serikali ya Marekani. Haya ni mafanikio makubwa kwa Sera yetu ya Mambo ya Nje na taifa kwa ujumla. |