Home » The Press » Taarifa kwa Vyombo vya Habari Kuhusu ziara ya Waziri Australia
RSS News
Taarifa kwa Vyombo vya Habari Kuhusu ziara ya Waziri Australia
Posted: Wednesday June 03, 2009 3:17 PM BT
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) leo ameanza ziara rasmi ya kiserikali ya siku 5 nchini Australia kwa mwaliko wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia, Mhe. Stephen Smith.

Akiwa nchini humo, Mhe. Membe atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake. Mazungumzo hayo yatalenga kukuza mahusiano baina ya Australia na Tanzania hususan katika sekta ya uchumi na jamii. Aidha Mhe. Membe baadaye leo anatazamiwa kukutana na Mabalozi walioko Canberra, Australia ambapo atatoa hotuba katika kuadhimisha siku ya Afrika.

Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Membe pia atakutana na Mwakilishi wa Malkia wa Uingereza nchini Australia (Governor General) Bi. Quentin Bryce na kutembelea Chuo Kikuu cha Western Australia ambapo atakuwa mgeni rasmi katika sherehe za kumbukumbu ya Siku ya Kimataifa ya Kulinda Amani (International Peacekeeping Day) tarehe 28/5/2009.

Mhe.Membe vilevile, atatembelea mgodi wa madini wa kampuni ya Barrick huko Perth na kufanya mazungumzo na viongozi wa mgodi huo. Pia atatembelea Hospitali ya King Edward Memorial ambapo atafanya mazungumzo na viongozi wa taasisi hiyo kuhusu mpango wa kupambana na vifo vya akina Mama na Watoto.

Mhe. Membe atarejea nchini tarehe 1 Juni 2009.


IMETOLEWA NA: WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA, DAR ES SALAAM

25 MEI, 2009