Resources » Press Release

UZINDUZI WA RIPOTI YA APRM

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

UZINDUZI WA RIPOTI YA APRM

Ripoti ya kwanza ya Utawala Bora iliyoandaliwa chini ya Mpango wa APRM kwa hapa Tanzania itazinduliwa rasmi na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 19 Julai 2017 hapa Dar es salaam.

APRM ni kufupi cha maneno ya ‘African Peer Review Mechanism’. APRM Tanzania ilipewa dhima na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kusimamia majukumu ya nchi yetu katika kuratibu tathmini ya utawala bora kwa mujibu wa miongozo ya Wakuu wa Nchi za Kiafrika.

Lengo la APRM ni kuzisaidia nchi za Kia-Afrika, Tanzania ikiwa mwanachama mmojawapo, kuhakikisha kuwa zinaimarisha utawala bora. Hii ni kwa kuwashirikisha wananchi wao kubainisha changamoto ili zigeuzwe kuwa fursa za maendeleo na mambo mazuri ya kuendelezwa kwa faida ya nchi yenyewe na hata kuwa mfano wa kuigwa na nchi nyingine.

Itakumbukwa kuwa Tanzania iliandaa Ripoti yake ya kwanza ya Utawala Bora chini wa Mpango wa Kujitathmini Ki-Utawala Bora (APRM) nakuiwasilishwa kwenye Kikao cha Wakuu wa Nchi wanaoshiriki Mchakato wa APRM mnamo Januari 2013, mjini Addis Ababa, Ethiopia. Kufuatia kukamilika kwa Ripoti hiyo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilianza utekelezaji wa kutatua changamoto za utawala bora zilizoainishwa kwenye Ripoti hiyo toka mwaka 2014, nao unafanyika na Wizara, Idara na Taasisi za Serikali kwa kupitia Mipango yao ya Muda wa kati. Taarifa za utekelezaji zinazoonyesha maendeleo yaliyofikiwa hadi sasa zimeendelea kutolewa katika maeneo ya, Muungano, Ardhi, Usawa wa Kijinsia na utoaji wa huduma mbalimbali za jamii kama elimu, afya, nishati, maji, Tehama na nyinginezo.

Uzinduzi wa Ripoti ya APRM ni utekelezaji wa mojawapo ya matakwa ya kiutaratibu katika Mchakato wa APRM, ikiwa ni kiashiria kimojawapo cha utekelezaji rasmi wa yale yaliyoandikwa kwenye Ripoti hiyo na pia kielelezo cha utayari wa Serikali katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Uzinduzi huo utakuhudhuriwa na wadau toka makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na; Viongozi waandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Viongozi Waandamizi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mawaziri wa pande zote mbili za Muungano, Makatibu Wakuu (JMT), Makatibu Wakuu (SMZ), Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baraza la Wawakilishi Zanzibar, majaji,mashirika ya kiraia, vyombo vya habari, vyama vya siasa, sekta binafsi, jumuiya za ushirika, Viongozi wa vijana, Viongozi wa wanawake, mashirika ya dini, wakulima, wasomi, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Tume za Uchaguzi,  na Washirika wa Maendeleo.

Mbali na wadau waliopo ndani ya nchi, uzinduzi huu pia utahudhuriwa na ujumbe toka Makao Makuu ya APRM yaliyopo Afrika Kusini. Kiongozi wa Ujumbe huo ni Mheshimiwa Brigitte Sylvia Mabandla, Mjumbe wa Jopo la Watu Mashuhuri na Kiongozi wa Mchakato wa Tanzania na Dakta Rachel Mukamunana, Mkuu wa Kitengo cha Tathmini za Nchi katika Sekretariati ya APRM na Mratibu wa Mchakato wa Tanzania.

Pamoja na kuwasilishwa kwenye kikao cha Wakuu wa Nchi za Afrika, hadi sasa Ripoti ya APRM pia imekwisha wasilishwa kwenye kikao chaBunge la Afrika huko Misri, mwezi Oktoba 2016. Katika vikao hivyo viwiwli, Wajumbe wengi waliisifia Tanzania hasa kwa kudumisha amani na utulivu, kulinda haki za binadamu,kuwa na Muungano uliodumu kwa zaidi ya miaka hamsini, maendeleo ya kiuchumi, matumizi ya lugha moja ya Kiswahili na hatua zilizopigwa katika utoaji wa huduma muhimu za kijamii.Pamoja na hatua hizo zilizopigwa na Tanzania, pia nchi ilishauriwa kuendelea kutatua changamoto zilibainishwa kwenye Ripoti ili hatimaye kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.

Mchakato wa APRM ni endelevu, na hivyo, taarifa za utekelezaji wa kuondoa changamoto zilizobainishwa kwenye Ripotiya APRM, ambazo zinaendelea kutatuliwa na Serikali, zitaendelea kuwasilishwa kwa wadau, na wakishazihakiki zitawasilishwa kwenye vikao vya Wakuu wa Nchi za Kiafrika.

 

Imetolewa na APRM Tanzania

Kwa Mawasiliano:

Sekretariati yaAPRM Tanzania,

Ghorofa ya 5 Jengo la Kitega Uchumi,

SLP  BOX 8315, DAR ES SALAAM.

tovuti: www.aprmtanzania.org

Email: aprm@aprmtanzania.org,

SIMU: +255 22 2129262/7…FAX: +255 22 213 5029