Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amewapangia vituo na kuwaapisha Mabalozi wapya wanne ambao uteuzi wao ulifanyika tarehe 03 Desemba 2016.

 • Mabalozi wapya wanne waapishwa na kupangiwa vituo

  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amewapangia vituo na kuwaapisha Mabalozi wapya wanne ambao uteuzi wao ulifanyika tarehe 03 Desemba 2016.

  Mabalozi hao ambao waliapishwa leo na Mhe. Rais Ikulu jijini Dar Es Salaam ni Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Dkt. Pindi Chana ambaye anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Mhe. John Haule. Mhe. Haule ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa iliyokuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alistaafu kwa mujibu wa sheria mwaka 2016.

  Mhe. Chana kabla ya kuteuliwa kuwa Balozi aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo Ubunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Unaibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto katika Serikali ya awamu ya nne.

  Balozi mwingine aliyeapishwa ni Mhe. Silima Kombo Haji anayekwenda kuwa Balozi wa kwanza wa Tanzania nchini Jamhuri ya Sudan baada ya Mhe. Rais kuamua kuufungua upya Ubalozi huo ambao ulifungwa miaka ya nyuma kutokana na sababu za kiuchumi. Kabla ya uteuzi huo Balozi Silima alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje Zanzibar katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

  Walioapishwa pia ni Mhe. Abdallah Kilima ambaye anakwenda nchini Oman kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Mhe. Ali Saleh aliyestaafu kwa mujibu wa sheria. Balozi Kilima kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa huo alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

  Balozi wa kwanza wa Tanzania nchini Jamhuri ya Korea, Mhe. Matilda Masuka naye aliapishwa na Mhe. Rais leo. Balozi Masuka kabla ya kukabidhiwa majukumu hayo mapya alikuwa Mkuu wa Utawala katika Ubalozi wa Tanzania nchini China. Jamhuri ya Korea ni moja kati ya nchi sita ambazo Mhe. Rais Magufuli amefungua Balozi mpya. Nchi nyingine ni Algeria, Jamhuri ya Sudan, Uturuki, Israel na Qatar.

  Imetolewa na:

  Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,

  Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

  Dar es Salaam, 26 Februari, 2017. • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Pindi Hazara Chana.

 • Mhe. Magufuli akimkabidhi vitendea kazi Balozi Chana

 • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Balozi wa Tanzania nchini Khartoum, Sudan Mhe. Silima Kombo Haji.

 • Mhe. Magufuli akimkabidhi vitendea kazi Balozi Silima

 • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Balozi wa Tanzania nchini Seoul, Korea Kusini, Mhe. Matilda Swila Masuka.

 • Mhe. Magufuli akimkabidhi vitendea kazi Balozi Masuka

 • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Balozi wa Tanzania nchini Mascut, Oman Mhe. Abdallha Abas Kilima.

 • Mhe. Magufuli akimkabidhi vitendea kazi Balozi Kilima

 • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (wa nne kutoka kushoto), Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Hassani Suluhu (wa tatu kutoka kushoto), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa Kasim Majaliwa (wa nne kutoka kulia), Katibu Mkuu Kiongozi Mhe Eng. John Herbert Kijazi (wa pili kutoka kushoto), Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Azizi Mlima (wa tatu kutoka kulia), wakiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi wateule mara baada ya kuapishwa, Ikulu jijini Dar es Salaam.

recommend to friends
 • Google+
 • PrintFriendly