Naibu Waziri afanya mazungumzo na Mabalozi Wateule

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Susan Kolimba amekutana na kufanya mazunguzo na Mabalozi Wateule wanaoenda kuiwakilisha Tanzania maeneo mbalimbali Duniani.Mazungumzo hayo yaliyofanyika ofisini kwake Makao Makuu ya Nchi mjini Dodoma, yalijikita katika kujadili namna bora ya kuiwakilisha Tanzania ughaibuni kwa kuzingatia sera ya nchi ya mambo ya nje,  kwa lengo la kuboresha mahusiano ya Kidiplomasia baina ya Tanzania na nchi hizo, na kwa kuzingatia maslahi mapana ya kiuchumi ya nchi yetu ikiwemo kutangaza shughuli za utalii zinazopatikana nchini.

Naibu Waziri Mhe. Dkt. Susan Kolimba akisisitiza jambo

Balozi Mteule Baraka H. Luvanda akichangia jambo wakati wa mazungumzo.

Punde baada ya mazungumzo na Mhe. Naibu Waziri, Mabalozi walikutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki 

Katibu Mkuu Wizara Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt.Aziz P Mlima akiongea na Mabalozi ofisini kwake mjini Dodoma


Mazunguzo yakiendelea

Wizara yajidhatiti kukarabati miundombinu ya Ofisi za Balozi

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Susan Kolimba akijibu swali la Mhe. Raisa Adallah Musa Bungeni katika kipindi cha maswali na majibu mapema leo asubuhi, amesema kuwa Wizara kwa kutumia bajeti ya maendeleo ya Serikali na vyanzo vingine vya mapato inaendelea kutekeleza mkakati wa kurekebisha na kuboresha miundombinu ya Ofisi za Balozi na makazi ya watumishi wa ubalozini katika maeneo mbalimbali yenye uwakilishi Duniani. Mkakati huu unahusisha ukarabati wa majengo yaliyopo, ujenzi wa majengo mapya, sambamba na ununuzi wa majengo mapya. Mkakati huu unaanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha ujao 2017/2018.  

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Susan Kolimba akijibu maswali kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge katika  Kikao cha Bunge kwenye kipindi cha maswali na majibu 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARITAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Watanzania waliokuwa wanashikiliwa nchini Malawi waachiwa huru

Mahakama Kuu ya Mzuzu nchini Malawi jana tarehe 12 Aprili 2017 iliwaachia huru Watanzania wanane waliokuwa wanashikiliwa nchini humo kwa kosa la kuingia kinyume cha sheria kwenye mgodi wa urani wa Kayerekera. 

Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Mzuzu, Bw. Texious Masoamphambe alitoa hukumu ya kifungo cha mwezi mmoja kwa kosa la kuingia kinyume cha sheria kwenye mgodi wa urani wa Kayerekera (trespass) na kifungo cha miezi mitatu kwa kosa la kufanya ujasusi (reconnaissance).

Makosa hayo mawili, kifungo chake kinakwenda pamoja na kwa mujibu wa Hakimu huyo watuhumiwa tayari wameshatumikia kifungo hicho na kuamuru waachiliwe huru. Aidha, Hakimu aliamuru Wizara ya Mambo ya Ndani na Usalama wa Ndani kuhakikisha kuwa Watanzania hao wanasafirishwa na kurejeshwa makwao haraka iwezekanavyo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi, Watanzania hao wamesafirishwa leo tarehe 13 Aprili 2017, kutoka Mzuzu hadi Mpaka wa Songwe/Kasumulu kati ya Tanzania na Malawi.  

Watanzania hao ambao ni Walasa Mwasangu, 30, Binto Materinus, 32, Ashura Yasiri, 63, Christian Msoli, 38, Layinali Kumba, 47, Maliyu Mkobe, Gilbert Mahumdi, 32, na Martin Jodomusole, 25 walikuwa wamekamatwa na kushikiliwa na vyombo vya usalama vya Malawi tokea tarehe 20 Desemba 2016.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 13 Aprili  2017.Balozi Asha-Rose Migiro awasilisha hati za utambulisho kwa Rais Michael D. Higgins wa Ireland

 Balozi wa Tanzania nchini Uingereza na Ireland, Dkt Asha-Rose Migiro mapema mwezi huu aliwasilisha hati za utambulisho (letter of credence) kwa Rais wa Ireland, Mhe. Michael D. Higgins.

Akiwasilisha hati hizo katika Ikulu ya Ireland, Balozi Migiro alimfikishia Rais Higgins salamu za Mhe. Rais John Magufuli na wananchi wa Tanzania pamoja na kumuahidi kufanya kazi itakayoimarisha uhusiano wa kihistoria baina ya Serikali za Tanzania na Ireland pamoja na kuanzisha maeneo mapya ya ushirikiano kwa kuzingatia vipaumbele vya Serikali ya awamu ya tano ya kujenga uchumi wa viwanda.

Balozi wa Tanzania nchini Uingereza na Ireland, Dkt Asha-Rose Migiro  akimkabidhi Rais Michael D. Higgins hati ya utambulisho kutoka kwa Mhe.Rais John Pombe Magufuli. 
Mhe. Balozi Migiro akikagua gwaride rasmi lililoandaliwa na kikosi cha Jeshi la Anga la nchi hiyo.
Balozi wa Tanzania nchini Uingereza na Ireland, Dkt. Asha-Rose Migiro  akiagana na Rais Higgins.
Mhe. Migiro  alitumia fursa hiyo pia kukutana na kuzungumza na wanadiaspora wa Tanzania waishio katika miji mbalimbali ya Ireland ambapo waliweza kujadili masuala mbalimbali kwa ajili ya ujenzi na maendeleo ya Taifa, hususan masuala ya uwekezaji na kutumia nafasi walizopata kuwa mabalozi wazuri katika kutangaza fursa zilizopo nchini sambamba na kudumisha utumaduni wetu.Pia Balozi Migiro aliwasihi wanadiaspora kushikamana, kuwa wamoja na kuunda Jumuiya ya Watanzania waishio Ireland akiwakumbusha kauli ya wahenga isimayo kuwa 'Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu'.